Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran amesema: "Iran itakabiliana na hatua ya Marekani ya kukiuka
majukumu yake katika utekelezaji wa mapatano ya nyuklia yajulikanayo kwa
jina la "Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA)."
Rais Rouhani ameyasema hayo leo alasiri mjini Tehran katika
kikao cha kimataifa cha waandishi habari kwa mnasaba wa kutumia mwaka
moja tangu kuanza kutekelezwa mapatano ya JCPOA.
Rais Rouhani ameashiria hatua ya Marekani ya kuvunja ahadi na
kuvuruga utekelezwaji wa mapatano ya nyuklia na kuongeza kuwa: "Serikali
na taifa la Iran litakabiliana kwa nguvu na uvunjaji ahadi huo na wala
halitalegeza msimamo kuhusu maslahi ya taifa."
Huku akiashiria mafanikio ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia na
nchi za kundi la 5+1 ambazo ni China, Russia, Ufaransa, Uingereza,
Marekani na Ujerumani, amesema: "JCPOA ni mafanikio makubwa kwa taifa la
Iran."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria suala la kuondolewa
Iran katika kipengee cha saba cha hati ya Umoja wa Mataifa na
kusema: "Urutubishaji madini ya urani ni haki ya taifa la Iran, na Umoja
wa Mataifa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA)
umetambua rasmi shughuli za nyuklia za Iran kwa malengo ya amani."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vikwazo vyote vya nyuklia
dhidi ya Iran viliondolewa baada ya kuanza kutekelezwa mapatano ya
nyuklia ya JCPOA yaliyotiwa saini Julai mwaka 2015 na kuanza kutekelezwa
Januari mwaka jana.
Rais Rouhani amesema Iran ni nchi yenye taathiri katika eneo la
Mashariki ya Kati na dunia na kuongeza kuwa: "Katika masuala mbalimbali
ya dunia, Iran ni nchi yenye nafasi muhimu na kutokuwepo Iran katika
masuala ya kisiasa ya kieneo ni hasara kwa dunia.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema chuki dhidi ya Iran
(Iranophobia) ni mbinu isiyo sahihi na kuongeza kuwa, Iran inataka
amani na usalama katika eneo hili na dunia nzima.
No comments:
Post a Comment