Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya
Iran, ametoa salamu za rambirambi kufuatia kufariki dunia Ayatullah
Hashemi Rafsanjani.
Ofisi ya kuhifadhi na kusambaza turathi za Kiongozi Muadhamu
imesambaza barua iliyoandikwa na Ayatullah Ali Khamenei kufuatia tukio
hilo chungu. Katika barua hiyo Kiongozi Muadhamu sanjari na kuonyesha
masikitiko yake makubwa kufuatia msiba huo, ametoa mkono wa pole kwa
familia na watu wa karibu wa mwanazuoni huyo, mwanamapambano, alimu na
mfuasi wa njia ya Imam Khomein (MA). Amesema na hapa ninamnukuu:
"Kumkosa Ayatullah Ali Akbar Hashemi Rafsanjani simtambui mtu mwingine
mwenye tajriba shirikishi na katika kipindi hiki kirefu nilichokuwa naye
nitamkumbuka hasa katika kipindi cha milima na mabonde ya kihistoria.
Hivi sasa mwanamapambano huyu mkongwe yupo mbele ya Mwenyezi Mungu
akiwa na faili lililojaa juhudi na harakati mbalimbali na hii ndio hatma
ya viongozi wote wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa moyo mkunjufu
ninamtakia maghfira, rehema na msamaha wa Mwenyezi Mungu na ninatoa pole
kwa mke, watoto, ndugu na marafiki wake wote." Mwisho wa kunukuu. Kati
ya nyadhifa ambazo Ayatullah Rafsanjani aliwahi kuzishika baada ya
ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran, Mwenyekiti wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya
Kiislamu (Bunge la Iran), Kaimu Amiri Jeshi Mkuu, Mwenyekiti wa Baraza
Kuu la Ulinzi wa Kitaifa na nafasi aliyoishika hadi kifo chake ya
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu.
No comments:
Post a Comment