Kiongozi mmoja wa mkoa wa Kivu Kusini nchini
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ametaka kuwepo mapambano ya
kukabiliana na wimbi la biashara za silaha kwa makundi ya wanamgambo
nchini humo.
Iciba Mboko mmoja wa viongozi wa serikali katika mkoa huo,
ameyasema hayo alipokutana na jumuiya za kiraia ambapo ametaka kuwepo
ushirikiano wa wananchi katika sekta za utumishi wa umma kwa ajili ya
kupambana na tatizo hilo sanjari na kuwataja watu wanaomiliki sihala
kinyume cha sheria.
Kadhalika Mboko amewataka wananchi kuwataja wamiliki wa maduka ya
silaha hizo ambazo zimekuwa zikitumiwa na makundi ya wabeba silaha
katika kuvuruga usalama na amani nchini. Akitoa maagizo hayo kwa wakazi
wa mji wa Bukavu, makao makuu ya mkoa wa Kivu Kusini, Iciba Mboko
ameongeza kuwa, umefika wakati wa raia na viongozi wa serikali
kushirikiana ili kurejesha usalama nchini humo.
Maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa yakishuhudia machafuko kwa kipindi cha
miaka 20 sasa. Kushindwa jeshi la serikali na kadhalika askari wa kofia
ya buluu wa Umoja wa Mataifa kuyatokomeza makundi ya wanamgambo,
inatajwa kuwa sababu ya kuendelea wimbi la machafuko hayo.
No comments:
Post a Comment