Rais Yahya Jammeh wa Gambia amekubali kuondoka madarakani kumpisha rais mpya Adama Barrow.
Kwa mujibu wa ripoti, Jammeh anaondoka nchini humo
kwenda kuishi uhamishoni, ingawa bado haijafahamika ni nchi gani
ataelekea. Habari za kuondoka rais huyo aliyetawala Gambia kwa miaka 22
sasa zimetolewa na rais anayetambuliwa na jamii ya kimataifa Adama
Barrow kupitia mtandao wake wa Twitter. Barrow ameeleza hayo baada ya
mazungumzo ya saa kadha yaliyokusudia kumshawishi Yahya Jammeh kukubali
matokeo ya uchaguzi wa tarehe Mosi Disemba mwaka jana.
Hii ni katika hali ambayo nchi kadhaa za Afrika Magharibi zimewatuma
wanajeshi wao nchini Gambia na kutishia kumuondoa Jammeh madarakani kwa
nguvu iwapo angekaidi amri ya kuachia madaraka kwa hiari. Barrow amekuwa
nchini Senegal kwa takriban wiki moja sasa ambapo pia aliapishwa kuwa
rais mpya wa Gambia katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Dakar Alkhamisi
iliyopita. Sasa Barrow anatambuliwa na jamii ya kimataifa kuwa kiongozi
mpya wa Gambia.
No comments:
Post a Comment