Rais mpya wa Gambia Adama Barrow amerejea
nchini kwake leo Alkhamisi akitokea nchi jirani ya Senegal, ambayo
alilazimika kuigeuza kimbilio lake tangu Januari 15, akihofia usalama
wake.
Mohammed Ibn Chambas, afisa wa Umoja wa Mataifa katika eneo la
magharibi mwa Afrika amewaambia waandishi wa habari nchini Senegal kuwa,
Barrow ameomba kikosi cha askari wa kieneo kisalie nchini humo kwa
miezi sita zaidi, hadi mambo yatakapotengamaa. Afisa huyo wa UN
ameongeza kuwa, uamuzi wa mwisho wa ombi la Rais Barrow utatolewa na
Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS.
Msemaji wa Barrow, Halifa Sallah amethibitisha kuwa, rais huyo mpya
wa Senegal anaingia nchini leo na kwamba sherehe za kumpokea zitafanyika
baadaye.
Rais Barrow anarejea Gambia baada ya kuondoka mtangulizi wake
aliyeiongoza nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika kwa miaka 22, Yahya
Jammeh.
Jammeh ambaye yuko uhamishoni nchini Equatorial Guinea, anadaiwa
kuondoka nchini Gambia na dola milioni 11 za Marekani kutoka hazina ya
taifa, tuhuma ambazo kiongozi mpya wa taifa ameagiza zichunguzwe.
Wananchi wa Gambia wana matarajio mengi kutoka kwa uongozi wa Barrow.
Tayari rais huyo mpya wa Gambia amemteua afisa wa zamani wa Umoja wa
Mataifa, Fatoumata Tambajang kuwa makamu wake.
No comments:
Post a Comment