Kamanda wa Jeshi la Gambia ametoa ujumbe
akitangaza uungaji mkono kamili wa jeshi la nchi hiyo kwa Rais Yahya
Jammeh ambaye amekataa kukabidhi madaraka ya nchi kwa njia ya amani
baada ya kushindwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika nchini humo mwezi
uliopita.
Taarifa hiyo imetangazwa na Jenerali Othman Badjie na kumuunga
mkono kiongozi huyo aliyeko kwenye mashinikizo makubwa ya kikanda ya
kimataifa yanayomtaka akabidhi madaraka kwa rais mteule wa Gambia, Adama
Barrow.
Rais Yahya Jammeh ambaye amekuwa madarakani kwa kipindi cha miaka 22
alishindwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwanzoni mwa mwezi
Disemba mwaka jana na kukubali matokeo yaliyompa ushindi hasimu
wake Adama Barrow. Hata hivyo siku chache baadaye aliibuka na kutilia
shaka matokeo hayo sanjari na kukataa kuondoka madarakani.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS)
imetishia kutuma vikosi vya kieneo nchini Gambia, iwapo Rais Yahya
Jammeh atakataa kukabidhi madaraka wakati muda wake utakapiomalizika
rasmi Januari 19 mwaka huu.
Jammeh amekataa kukabidhi madaraka kwa rais mteule akidai kuwa zoezi
la uchaguzi wa mwezi uliopita nchini Gambia lilitawaliwa na dosari
nyingi na anataka uchaguzi wa rais ufanyike tena.
No comments:
Post a Comment