Burundi imetishia kuushataki Umoja wa Afrika-AU na wakati huohuo kutishia kuwaondoa askari wake waliopo katika nchini ya Somalia ambao wanaohudumu chini ya
mwavuli wa Kikosi cha Kulinda amani cha Umoja wa Afrika- Amisom.
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi amesema askari wa nchi hiyo
wanaohudumu katika kikosi cha Amisom hawajalipwa mishahara na marupurupu
yao kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na ndiposa serikali yake inataka
kuwaondoa nchini Somalia, mbali na kuishtaki AU.
Amesema iwapo kadhia hiyo ya mshahara haitakua imepatiwa ufumbuzi
kufikia mwezi ujao, serikali yake haitakuwa na chaguo jingine ghairi ya
kuwaondoa askari wa nchi hiyo Somalia.
Burundi ambayo ina askari 5,432 ndani ya Amisom, ni nchi ya pili
baada ya Uganda kwa kuwa na idadi kubwa ya askari wa kulinda amani
nchini Somalia.
Rais wa Burundi amesema nchi hiyo itaushtaki Umoja wa Afrika kwa
kukiuka muafaka uliofikiwa na pande zote kuhusiana na mishahara ya
askari wa Amisom.
Amisom ilijikuta katika kipindi kigumu cha kuwalipa mishahara
wanajeshi zaidi ya 22 elfu wa nchi za Afrika zilizotuma askari wake
Somalia zikiwa ni pamoja na Kenya, Ethiopia na Djibouti, baada ya Umoja
wa Ulaya EU kupunguza bajeti yake kwa kikosi hicho cha kulinda amani,
kwa asilimia 20 mapema mwaka huu.
Nchi ya Somalia iliyoko katika Pembe ya Afrika imekuwa ikikabiliwa na
machafuko kwa miaka kadhaa sasa huku kundi la wanamgambo wa al-Shabaab
likitishia pakubwa usalama wa nchi hiyo na hata wa nchi jirani.
No comments:
Post a Comment