Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
limetangaza katika kikao chake kilichofanyika usiku wa kuamkia leo
kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza majukumu yake yote
kuhusu makubaliano ya nyuklia kati ya Tehran na kundi la 5+1 maarufu kwa
kifupi kama JCPOA.
Mwakilishi wa Ulaya katika kikao cha jana cha Baraza la Usalama
kilichofanyika kuchunguza jinsi Iran ilivyotekeleza makubaliano ya
JCPOA, amesema kuwa Baraza la Usalama litapokea tena ripoti kuhusu faili
hilo miezi sita ijayo. Afisa huyo wa Umoja wa Ulaya amemnukuu Mkuu wa
Siasa za Nje wa Umoja huo Bi Federica Mogherini akisema kuwa,
makubaliano ya nyuklia ya Iran sasa ni makubaliano ya kimataifa.
Kwa upande wake mwakilishi wa Ufaransa amesema katika kikao hicho cha
UN kwamba, uhusiano wa nchi yake na Iran umeboreka baada ya makubaliano
ya JCPOA. Mjumbe wa Uingereza ambaye pia amehutubia kikao hicho amesema
ulimwengu uko tayari kushirikiana zaidi na Iran katika masuala ya
kiuchumi.
Hata hivyo kauli ya Umoja wa Mataifa kwamba Iran imetekeleza
kikamilifu majukumu yake kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
hayakuifurahisha Marekani. Mwakilishi wa serikali ya Washington katika
Umoja wa Mataifa, Samantha Power ameendeleza uhasama wa miaka mingi wa
Marekani dhidi ya Iran na kusema kuwa, makubaliano ya JCPOA hayapasi
kulifanya Baraza la Usalama lisizingatie masuala mengine ya Iran.
Samantha Power amedai katika kikao hicho kwamba Iran imekiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa yanayohusiana na silaha.
No comments:
Post a Comment