Milio ya risasi imesikika katika mji uliokumbwa na hali ya mchafukoge wa Bouaké, huko kaskazini mwa Côte d’Ivoire.
Ufyatuaji risasi huo umetokea katika hali ambayo mazungumzo ya
siku mbili baina ya Alain Richard Donwaki Waziri wa Uulinzi na askari
waasi yangali yanaendelea mjini hapo. Kwa mujibu wa mashuhuda, risasi
zimesikika karibu na kituo cha utamaduni ambako imepangwa kuwa Richard
Donwaki na kiongozi wa askari hao waasi watakutana kwa ajili ya
mazungumzo hayo.
Wakati huo huo, askari waliopo katika mji wa Daloa katikati mwa Côte
d’Ivoire wamefyatua risasi angani suala ambalo limewafanya
wafanyabiashara wa mji huo kufunga maduka yao kwa kuhofia usalama wao.
Uasi wa askari nchini Côte d’Ivoire uliibuka tarehe sita mwezi huu
katika mji wa Bouaké na kusambaa haraka katika miji mingine ya Ivory
Coast ukiwemo mji wa kiuchumi wa Abidjan. Hii ni katika hali ambayo
serikali ya Yamoussoukro, imeahidi kutekeleza matakwa ya askari hao
ikiwa ni pamoja na kuongeza mishahara yao, kuwalipia bima na makazi.
Kufuatia uasi huo, Rais Alassane Ouattara aliwapiga kalamu nyekundu
makamanda wa jeshi na polisi nchini humo. Kwa mujibu wa weledi wa mambo
machafuko hayo mapya yatazorotesha juhudi za rais huyo za kujaribu
kutuliza hali ya mambo nchini.
No comments:
Post a Comment