Watu wasiopungua 36 wameuawa na wengine wengi
kujeruhiwa leo kufuatia hujuma ya kigaidi katika kitongoji cha Sadr
katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.
Duru za usalama Iraq zinasema
hujuma hiyo ilitokea katika kituo cha mabasi katika kitongoji cha Sadr
ambacho wakaazi wake wengi ni Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Kundi la kigaidi la ISIS au Daesh
limetoa taarifa na kudai kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi ambayo
imewalenga raia wasio na hatia.
Kwingineko magaidi wa ISIS wameshambulia
kwa kombora katika mtaa wa Al Tamim mashariki mwa mji wa Mosul
kaskazini mwa Iraq kuwaua raia 18.
Huku hayo yakijiri, vikosi vya kujitolea
vya wananchi wa Iraq vimetoa taarifa na kusema vimefanikiwa kuzuia
hujuma za magaidi katika mikoa ya Najaf al Ashran na Karbala.
Imedokezwa kuwa magaidi hao walikusudia
kuingia katika mikoa hiyo miwili kwa kupitia eneo la An Nakhib ambapo
kulijiri mapigano baina ya magaidi na vikosi vya kujitolea vya wananchi
na kupelekea magaidi sita kuuawa.
Hayo yanajiri katika hali ambayo,
viongozi wa Iraq wameendelea kusisitiza azma ya serikali ya nchi hiyo ya
kupambana na makundi ya kigaidi kwa hali na mali hadi itakapong'oa
mizizi ya magaidi yao katika ardhi ya nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment