Wabunge wa chama cha Republican katika bunge
la Marekani wanaandaa barua ya kumpelekea rais mteule wa nchi hiyo
Donald Trump wakitaka serikali mpya ijayo ichukue hatua haraka ya
kuuhamishia Baitul Muqaddas ubalozi wa nchi hiyo ulioko Tel Aviv.
Barua
hiyo hadi sasa imeshasainiwa na wabunge 100 wa chama cha Republican
katika Bunge la Wawakilishi huku ikiendelea kusambazwa ili kupata idadi
kubwa zaidi ya watakaoisaini.
Sehemu
moja ya barua hiyo inamtaka Tump kuchukua hatua ya haraka mara baada ya
kushika hatamu za uongozi ya kuuhamishia Quds tukufu inayokaliwa kwa
mabavu ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv, mji mkuu wa utawala haramu
wa Israel.
Sehemu ya barua hiyo ya wabunge wa chama cha Republican inaeleza
kuwa: "Kuuhamisha ubalozi huo kutaimarisha muungano wa kipekee uliopo
baina ya Israel na Marekani na kufikisha ujumbe wa wazi kwa dunia kwamba
tunaiunga mkono Israel kwa kuitambua Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu
wake wa milele.
Tarehe 5 ya mwezi huu wa Januari, Jordan, ambayo inasimamia
uendeshaji wa eneo la msikiti mtukufu wa Al-Aqsa katika Baitul Muqaddas
Mashariki ilimtahadharisha Donald Trump juu ya matokeo ya "balaa" endapo
ataamua kutekeleza ahadi aliyotoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais
wa Marekani ya kuuhamishia Quds tukufu inayokaliwa kwa mabavu ubalozi
wa nchi hiyo ulioko Tel Aviv. Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO)
nayo pia imeionya Marekani juu ya hatua hiyo na kueleza kwamba balozi
zote za Marekani katika Ulimwengu wa Kiarabu itapasa zifungwe kutokana
na ghadhabu za wananchi wa mataifa ya Kiarabu dhidi ya hatua hiyo…/
No comments:
Post a Comment