Tokea aage dunia Hashimi Rafsanjani, Mkuu wa
Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran hapo siku
ya Jumapili jioni, vyombo vya habari na duru nyingi za kisiasa za
kimataifa zimekuwa zikichambua kwa kina historia na maisha ya shakhsia
huyo muhimu.
Bila shaka jambo hilo linabainisha wazi nafasi muhimu na
maalumu aliyokuwa nayo Hashimi Rafsanjai katika mfumo mzima wa Mapinduzi
ya Kiislamu hapa nchini na kwamba kuaga kwake dunia bila shaka ni msiba
mkubwa kwa mfumo huu. Vyombo hivyo vya habari ikiwemo BBC ambayo
ilikatiza ratiba zake za kawaida za utangazaji na kurusha hewani vipindi
maalumu vya historia ya Mapinduzi ya Kiislamu na maisha pamoja na
nafasi ya Hashimi Rafsanjani katika mapinduzi hayo, vilidai kwamba
mazishi ya Rafsanjani yanaweza kuchambuliwa katika mitazamo miwili,
mmoja ukiwa ni kwamba mazishi yake ni ya kiserekali na wa pili ni kwamba
ni fursa kwa wale wasioridhishwa na hali ya mambo au wanaounga mkono
misimamo na mitazamo yake, hasa mwishoni mwa umri wake, kudhihirisha
matakwa yao hadharani. Muelekeo huo wa kihabari ambao umekuwa
ukifuatiliwa na vyombo vingi vya habari vya magharibi unataka
kuthibitisha kwamba kumekuwepo na hitilafu za mitazamo kati ya marehemu
Rafsanjani na viongozi wengine wa Mfumo wa Kiislamu.
Pamoja na hayo hata tukifaradhisha kuwepo kwa hitilafu na tofauti
kama hizo za kimtazamo kuhusiana na baadhi ya sera za kisiasa za
Rafsanjani, kwa hakika jambo hilo halipaswi kupingwa wala kuchukuliwa
kuwa baya, bali hiyo ni moja ya nukta muhimu na chanya katika muundo wa
Mfumo wa Mapinduzi ya Kiislamu, nukta ambayo inathibitisha wazi uwezo na
uvumilivu mkubwa uliopo miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa mfumo
huu. Hakuna shaka yoyote kwamba Hashimi Rafsanjani katika hilo ameweza
kudhihirisha mfano bora na kuthibitisha kwa maneno na vitendo kwamba
licha ya kuwa na mitazamo tofauti na huru kuhusiana na baadhi ya mambo
lakini wakati huohuo inawezekana kusalia kwenye misingi na hivyo kulinda
umoja wa kitaifa na kuifanya sheria kuwa kigezo kinachopasa kufuatwa na
kuzingatiwa na wote katika uchukuzi wa maamuzi. Alithibitisha wazi
suala hilo wakati alipoamua kutii sheria na kutovuka mistari myekundu ya
sheria kwa kuafikiana na uamuzi wa mahakama wakati mtoto wake mwenyewe
alipohukumiwa kwenda jela kutokana na baadhi ya masuala ya kisheria.
Kwa msingi huo tunapasa kusema kuwa hitilafu za mitazamo ni jambo
linalopasa kuwepo katika kila jamii yenye harakati na uhai la sivyo
jamii hiyo hupoteza uhai huo. Sula muhimu hapa ni jinsi ya kulitazama
jambo hilo. Hii ni nukta ambayo Rafsanjani mwenyewe amekuwa akiisisitiza
mara kwa mara na hasa baada ya matukio ya fitna ya 2009 ambapo licha ya
kuwa na msimamo tofauti kuhusiana na matukio hayo lakini alisisitiza
sana kulindwa thamani za Mfumo wa Kiislamu na kufuatwa amri za Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa mtazamo huo Ayatullah Hashimi
Rafsanjani alilichukulia suala la umoja kuwa nguzo muhimu ya kulindwa
mfumo huu na kigezo cha kutathminiwa tabia na misimamo ya kisiasa katika
vipindi muhimu vya Mapinduzi ya Kiislamu. Alikuwa akiamini kwa dhati
kwamba Mapinduzi na Mfumo huu ni wa wananchi wote na kwamba mirengo yote
ya kisiasa na kifikra nchini inapata uhalali wao kutokana na uungaji
mkono wa wananchi na kwa hivyo maslahi yao ya kitaifa hayapasi kufanywa
kuwa muhanga wa maslahi ya kisiasa ya watu maalumu. Katika miaka ambayo
nchi iliathirika kutokana na matokeo ya uchaguzi wa rais wa duru ya
kumi, alichambua mambo mbali kabisa na hisia na ushabiki wa kisiasa na
kujaribu kutuliza mivutano na kuielekeza kwenye mkondo wa sheria. Hata
kama alikuwa na mitazamo na matatizo fulani kuhusiana na hali
iliyojitokeza nchini katika kipindi hicho lakini alikuwa akiyawasilisha
na kuyazungumzia katika ngazi za juu za mfumo na sio kuropokwa ovyo ili
kulinda umoja na mshikamano wa kitaifa.
Katika upande wa pili vyombo vya habari vya kigeni ambavyo havijasita
kufanya njama za kuonyesha kuwepo mgawanyiko mkubwa miongoni mwa
viongozi wa ngazi za juu wa Mfumo wa Kiislamu mara hii pia vimejaribu
kutumia fursa ya kifo cha Hashimi Rafsanjani kujaribu tena kusisitiza
suala la kuwepo hitilafu kubwa kati ya marehemu na viongozi wengine wa
ngazi za juu wa Mfumo wa Kiislamu. Hii ni katika hali ambayo Rafsanjani
mwenyewe katika utekelezaji wa majukumu yake ya kimapinduzi alikuwa
akiuzingatia sana mustakbali wa Mfumo wa Kiislamu na nchi nzima kwa
ujumla na hasa kuhusiana na suala zima la uongozi wa masuala ya kiuchumi
na kisiasa ili kuimarisha nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu. Akiwa
mwanamapinduzi halisi na shakhsia muhimu na mwenye busara wa kisiasa
nchini, Ayatullah Rafsanjani aliweza kutekeleza ipaswavyo na kivitendo
majukumu aliyokuwanayo na hivyo kutoa mchango mkubwa katika kulinda
Mapinduzi ya Kiislamu na kukabidhi thamani zake kwa vizazi vijavyo vya
mapinduzi hayo.
No comments:
Post a Comment