Leo tarehe Pili Januari umetimia mwaka mmoja
tangu utawala wa kifalme wa Saudi Arabia umuue kikatili mwanazuoni
mashuhuri na mtetezi mkubwa wa haki za binadamu nchini humo Sheikh Nimr
Baqir al Nimr.
Kwa mnasaba huo wapinzani wa utawala wa Kifalme wa Saudia
wamefanya maandamano katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo na katika
miji kadhaa ya nchi za kigeni huku wadau wa mitandao ya kijamii
wakilaani na kumkumbuka msomi huyo aliyesimama kidete kupigania haki za
wanaodhulimiwa.
Sheikh Baqir al Nimr alikamatwa na vyombo vya usalama vya Saudi
Arabia Julai mwaka 2012 kufuatia maandamano makubwa yaliyofanyika
Februari 2011 katika eneo lenye Waislamu wengi zaidi wa madhehebu ya
Shia la Qatif huko mashariki mwa Saudia. Tarehe 15 Oktoba 2015 Mahakama
ya utawala wa Aal Saud ilimhukumu kifo mwanazuoni huyo wa Kiislamu kwa
tuhuma zisizo na msingi eti za kuhujumu usalama wa taifa na hatimaye
msomi huyo aliuawa kwa kukatwa kichwa na mwili wake ukasulubiwa.
Mauaji ya Sheikh Baqir al Nimr ambayo yalitambuliwa kuwa ni jinai ya
kutisha na ugaidi wa kiserikali, yalilaaniwa sana na jumuiya za kikanda
na kimataifa za kutetea haki za binadamu. Ili kuficha na kutaka
kuhalalisha mauaji ya mwanamapambano huyo, utawala wa Saudi Arabia pia
uliwanyonga na kuwaua vijana kadhaa pamoja na Sheikh Nimr ambao walikuwa
wakikabiliwa na tuhuma za ugaidi.
Mbinyo na ukandamizaji wa serikali ya Saudia dhidi wananchi hususan
Waislamu wa madhehebu ya Shia, unaongezeka siku baada ya siku na askari
usalama wa nchi hiyo wamezidisha mashambulizi dhidi ya wakazi wa maeneo
ya mashariki. Kwa vyovyote vile, hali ya Saudia na malalamiko
yanayoongezeka kila uchao ya wananchi dhidi ya watawala na jinai
zinazofanywa na Aal Saud hususan mauaji ya Sheikh Nimr, ni miongoni mwa
makosa ya kistratejia ya utawala huo ambayo taathira zake zimezidisha
matatizo ya utawala huo wa kifalme na kutikisa nguzo zake.
Duru za kisheria pia zimekuwa zikilaani mauaji ya mpigania haki huyo
mashuhuri na kusisitiza kuwa, msomi huyo aliuawa kwa sababu tu ya
kukosoa utawala wa Saudia na kupinga dhulma na ukandamizaji, jambo
ambalo si kosa la kumfanya mtu auawe kwa kukatwa kichwa. Wadadisi wa
mambo wanasema, utawala wa Saudia unatumia hukumu za kifo na kukata watu
vichwa kama wenzo wa kunyamazisha wapinzani wake na kujenga mazingira
ya hofu ili kuwatisha na kuwazua wapinzani kukosoa utendaji na dhulma za
utawala huo. Hata hivyo na licha ya ukandamizaji huo dhidi ya
wapinzani, maandamano na malalamiko dhidi ya Aal Saudi yamekuwa
yakishadidi siku baada ya siku. Suala hili linaonesha kuwa, mbinu za
kujenga mazingira ya hofu na ukandamizaji zimeshindwa kuwanyamazisha
wapinzani na harakati ya mwamko wa wananchi huko Saudi Arabia.
Kwa hakika damu ya mpigania haki na uadilifu huyo imezidisha mori na
vuguvugu la mwamko la watu dhidi ya ukandamizaji wa Saudi Arabia na
hapana shaka kuwa Sheikh Nimr Baqir al Nimr ataendelea kukumbukwa katika
harakati zote za kudai haki na kupinga dhulma na ukatili wa watawala wa
Aal Saud.
No comments:
Post a Comment