Viongozi wa China wamesema kuwa, indhari ya
kutokea vita kati ya nchi hiyo na Marekani katika kipindi cha Rais
Donald Trump, sio madai pekee, bali ni ukweli halisi.
Afisa mmoja wa ngazi ya juu katika jeshi la China ambaye
hakutaka kutaja jina lake sambamba na kusema maneno hayo ameongeza kuwa,
katika kujiandaa na vita na Marekani, jeshi la nchi hiyo limeweka mfumo
wa ulinzi wa makombora katika bahari ya kusini na mashariki mwa China,
kwa ajili ya ulinzi wa Peninsula ya Korea. Afisa huyo wa jeshi la China
amesisitiza kuwa, Beijing imeingia katika awamu mpya ya kujiimarisha
kiulinzi kutokana na hatari inayolikabili eneo la kusini mashariki mwa
Asia.
China imechukua hatua hizo kutokana na matamshi ya uhasama ya rais
mpya wa Marekani Donald Trump dhidi ya nchi hiyo. Hivi karibuni pia
jeshi la China lilitangaza kuwa, kuendelea kuwa mbaya hali ya mambo
kuhusiana na usalama wa bahari ya eneo, machafuko katika eneo la Asia na
Bahari ya Pasifiki na kadhalika misimamo tata ya rais huyo mpya wa
Marekani, inailazimu kujiandaa kuingia katika vita tarajiwa na Marekani
kuliko wakati mwingine wowote ule.
Ripoti hiyo ya jeshi la China ilifafanua kuwa, msimamo wa Washington
wa kuweka ngao ya makombora ya THAD nchini Korea Kusini, kuongeza idadi
ya askari wake katika maeneo ya mashariki na kusini mwa bahari za Uchina
na kadhalika kuanzisha mlingano mpya wa kijeshi barani Asia, ni siasa
ambazo zinaweza kuwasha moto wa vita wakati wowote. Mwezi Disemba mwaka
jana, Donald Trump alitangaza kuwa, Washington haitafungamana na siasa
za 'China Moja' kuhusiana na uhusiano wa nchi yake na Taiwan, suala
ambalo lililalamikiwa na Beijing.
Hii ni kwa kuwa mara kadhaa Beijing imekuwa ikitangaza kuwa, siasa za
'China Moja' ni suala lisilo na mjadala huku ikiitaka Washington
kuangalia upya siasa zake kuhusiana na suala hilo.
No comments:
Post a Comment