Tuesday, May 23, 2017

SAUDIA MNUNUZI MKUBWA ZAIDI WA SILAHA ZA MAREKANI, ISRAEL MPOKEZI MKUBWA ZAIDI WA MISAADA YA KIJESHI YA MAREKANI

Utawala wa Kizayuni wa Israel umebainisha wasiwasi wake kuhusu Marekani kuiuzia Saudi Arabia silaha zenye kugharimu mabilioni ya dola katika hali ambayo Israel yenyewe inapokea misaada ya silaha za kisasa zaidi kutoka Marekani.
Yuval Steinitz Waziri wa Nishati wa Israel Jumapili alibainisha wasiwasi wake kuhusu mkataba wa Marekani kuiuzia Saudia silaha zenye thamani ya mabilioni na dola na kudai kuwa mkataba huo uteiletea Israel matatizo. 
Jumamosi Mei 20 Rais Donald Trump wa Marekani aliwasili Saudia na hadi Mei 22 alipoondoka Riyadh na kuelekea Tel Aviv kukutana na wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Moja ya matukio muhimu zaidi ya safari ya Trump mjini Riyadh ni kutiwa saini mkataba wa ununuzi silaha zenye thamani ya dola bilioni 350 na hilo ndilo lililomtia wasi wasi waziri wa nishati wa utawala wa Israel. Lakini je, ni kweli kuwa mkataba huo wa silaha utakuwa na taathira hasi kwa Israel hadi kufikia kiwango cha waziri huyo au wengine kuwa na wasi wasi kiasi hicho?
Uhusiano wa Israel na Saudia katika miaka ya hivi karibuni umetoka katika kiwango cha 'uhasama' na kuwa wa 'mashindano'. Kwa hivyo hata kama mikataba ya kijeshi ya Marekani na Saudia inaitia Israel wasiwasi si kwa kiwango cha kutisha. Aidha uhusiano wa karibu wa Israel na Saudi Arabia umezidi kudhihirika katika miaka ya hivi karibuni baada ya maafisa wa tawala hizo mbili kukutana maeneo mbali mbali.
Trump na Salman wakitia saini mapatano ya kuiuzia Saudia silaha
Nukta nyingine ni kuwa ingawa Israel na Saudia ni waitifaki wakubwa zaidi wa Marekani Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) lakini ukweli ni kuwa Israel inapewa uzito na umuhimu mkubwa zaidi na Marekani kuliko Saudia. Ni kwa msingi huo ndio maana Marekani haiwezi kuchukua hatua yoyote yenye kutia hatarani usalama wa utawala haramu wa Israel.
Maudhui nyingine hapa ni kuwa, pamoja na kuwa Marekani imeafiki kuiuzuia Saudi Arabia silaha zinazogharimu mabilioni ya dola lakini katika upande wa pili inaipatia Israel silaha za kisasa kabisa ambazo katu haiwezi kuiuzia Saudia.
Kwa hivyo katika hali ambayo Marekani inachangia kueneza hofu na chuki dhidi ya Iran na kwa msingi huo kuibua adui bandia ili kuishawishi Saudia na madola mengine ya Kiarabu yanunue silaha za Kimarekani lakini kile ambacho ni muhimu kwa Marekani ni uhusiano wake na Israel ambao umejengeka katika msingi wa  'kufungamana na kulinda usalama' wa utawala huo.
Nukta ya nne hapa ni kuwa makubaliano ya Marekani kuizuia Saudia silaha kimsingi ni kwa faida ya Marekani. Kama alivyotamka Trump baada ya kutiwa saini mapatano hayo, Marekani imeweza kuvutia uwekezaji wa Saudia na hilo litapelekea Wamarekani kupata ajira. Kimsingi ni kuwa Marekani inapora utajiri wa mafuta wa Saudia kwa kuipatia silaha duni na kwa bei ya juu huku ikiipatia Israel msaada wa silaha za kisasa kabisa.
Ikumbukwe kuwa Septemba mwaka 2016, Marekani na Israel zilitiliana saini mapatano makubwa zaidi ya kijeshi. Kwa mujibu wa mapatano hayo, Marekani iliahidi kuwa, katika kipindi cha miaka 10 ijayo, itaipatia Israel msaada wa kijeshi wenye thamani ya dola bilioni 38.
Ndege za kivita aina ya F18 zilizotengenezwa Marekani
Ukweli ni kuwa mkataba wa kijeshi wa Marekani na Saudia hautakuwa na athari yoyote mbaya kwa Israel na hatua ya waziri wa nishati wa Israel kudai kuwa eti ana wasi wasi ni kwa ajili tu ya kuishinikiza Marekani iupe utawala huo misaada zaidi.
Mkataba wa kijeshi wa Marekani na Saudia una malengo na manufaa ya  kiuchumi zaidi kuliko ya kijeshi kama ambavyo pia utawala wa Kizayuni wa Israel umetia saini mkataba wa kuiuzia India mfumo wa kujihami angani wenye thamani ya dola milioni 630. India pia imetiliana saini mapatano mengine ya miaka 10 na shirika moja la kijheshi la Israel.

No comments:

Post a Comment