Brigedia Jenerali Hussein Dehqan
Televisheni ya al-Manar ya nchini Lebanon
imemnukuu Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisema kuwa
iwapo Saudi Arabia itachukua hatua yoyote ya kipumbavu dhidi ya Iran,
hakuna sehemu yoyote ya nchi hiyo itakayokuwa salama isipokuwa miji
mitakatifu ya Makka na Madina tu.
Al-Manar imemnukuu Brigedia Jenerali Hussein Dehqan, Waziri wa
Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiionya Riyadh kuwa, kiburi cha
watawala wa Saudia kimewapelekea kutamka maneno ambayo wao wenyewe
hawatambui uzito wake na kwamba kubwa zaidi wanaloweza kulifanya ni
kuuchochea utawala haramu wa Israel dhidi ya Iran.
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema hii leo Saudia imekata tamaa kiasi
cha kuifanya ijidhalilishe na kumsifu Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa
utawala ghasibu wa Israel. Hakuna wakati wowote ambapo Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran imekuwa na nia ya kuteka au kuichokoza nchi nyingine
lakini imekuwa ikitangaza mara kwa mara kwamba haitasita kutoa jibu
dhidi ya mchokozi yeyote na kwamba ina nguvu za kutosha za kuweza
kuepusha vitishio na pia kutoa jibu kali la majuto dhidi ya adui
mchokozi.
Watawala wa Saudia ambao wameutumbukiza ulimwengu mzima wa Kiislamu
katika lindi la vita, machafuko na fikra za kuchupa mipaka badala ya
kukiri makosa yao wameanza kuitisha Iran kwa vitisho ambavyo vyenyewe ni
vikubwa kuliko uwezo wao. Kizazi kipya cha watawala wa Saudia kinyume
na walivyokuwa watangulizi wao ambao kidogo walikuwa wakitahadhari
katika kukabiliana na masuala ya eneo, kimeamua kwa pupa kuwa mstari wa
mbele wa kukabiliana na masuala hayo bila ya kuchukua tahadhari yoyote
ya lazima. Kizazi hicho ambacho kinaoongozwa na Muhammad bin Salman,
Naibu Mrithi wa Kiti cha Ufalme na ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi wa
Saudi Arabia kinaamini kwamba nchi hiyo inapasa kuwa na nafasi yake
halisi katika eneo kwa kuchukua hatua za kijasiri na kishujaa zaidi.
Kutumwa wanajeshi wa Saudia nchini Bahrain kwa ajili ya kuwakandamiza
Mashia wa nchi hiyo, uvamizi wa nchi hiyo huko Yemen kwa ushirikiano wa
Marekani na utawala ghasibu wa Israel, maafa ya Mina katika msimu wa
Hija na kuuawa kidhulma Sheikh Nimr, mwanazuoni mashuhuri wa Saudia ni
ishara zinazobainisha wazi utambulisho halisi wa watawala hao wapya wa
ukoo wa Aal Soud. Muhammd bin Salman amethibitisha wazi kwamba kwa
msingi wa sera mpya za Saudi Arabia za kufuatilia siasa za hujuma,
anataka kulitwisha eneo hili fikra kwamba Riyadh ndiyo nguvu kubwa zaidi
katika eneo hili la Mashariki ya Kati.
Utangazwaji wa uwepo huo wa nguvu wa Saudia unakamilishwa na hatua ya
Bin Salman ya kujiunga na kambi ya Marekani, Uingereza na utawala
haramu wa Israel katika eneo. Hii ni katika hali ambayo Saudia
inakabiliwa na migogoro chungu mzima ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama
ambayo inaweza kusambaratisha kirahisi nguzo zilizozeeka za utawala wa
kifalme nchini humo. Mbali na hayo sehemu kubwa ya siasa za Saudia
zimesimama juu ya msingi wa kuudhaminia usalama utawala wa Kizayuni wa
Israel katika eneo hili muhimu la Mashariki ya Kati. Pamoja na huduma
hiyo yote kwa utawala huo haramu, lakini watawala wa Riyadh bado wana
wasiwasi wa kuendelea kuitegemea Marekani kupita kiasi na kwa hivyo
wameamua kuanzisha chokochoko na kubuni mbinu mpya za kubadilisha hali
ya mambo katika eneo. Lakini ukweli wa mambo ni kuwa mfumo wa kisiasa wa
Saudi Arabia umeshindwa kuendana na matukio ya hivi sasa ya kieneo na
kimataifa na hivyo kushindwa siasa zake za uingiliaji katika eneo.
Pamoja na hayo lakini bado watawala wa Saudia wanadhani kwamba
wanaweza kufidia nafasi yao iliyodhoofika katika eneo kwa kuanzisha
siasa za uchokozi, uhasama na hujuma dhidi ya nchi nyigine, jambo ambalo
bila shaka ni ndoto tu. Kile wanachopasa kukifahamika vyema watawala wa
Saudia kimebainishwa wazi na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran katika sentensi fupi lakini iliyobeba ujumbe mzito, aliyoitakamka
wakati wa kuhojiwa na televisheni ya al-Manar ya nchini Lebanon. Hivyo
basi kama kizazi kipya cha watawala wa Saudia kitakuwa na chembe ya
busara bila shaka kitalazimka kutafakari na kufahamu vyema iliko nafasi
yake katika eneo, kwa sababu hata mabwana zao yaani Marekani na Israel
hawana uwezo wa kuishambulia Iran. Hii ni kwa sababu wakiamua kuchukua
hatua yoyote ya kipumbavu na kishenzi bila shaka watatumbukia kwenye
shimo refu lisilo na kina ambapo itawawia vigumu kujinasua humo.
No comments:
Post a Comment