Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Thursday, May 11, 2017

UN: DOLA MILIONI 900 ZAHITAJIKA KUNUSURU MAISHA YA WASOMALI MILIONI 6

Umoja wa Mataifa umesema unahitajia dola milioni 900 za Marekani kufikia mwishoni mwa mwaka huu kwa ajili ya kunusuru maisha ya raia milioni 6 wa Somalia wanaohitajia misaada ya dharura ya kibinadamu.
Akiongea katika ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa kuhusu Somalia linalofanyika katika mji mkuu wa Uingereza, London hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema Wasomali milioni 6 wanahitajia misaada ya kibinadamu haraka iwezekanavyo, wakiwemo watoto wadogo zaidi ya laki 2 na 75 elfu, wanaosumbuliwa na utapiamlo na lishe duni.
Amesema watoto wa Kisomali wanakodolewa macho na uhaba wa chakula, maji sambamba na magonjwa mbalimbali yaliyosababishwa na mazingira machafu.
Rais Farmajo akihutubu katika Kongamano la London
Taarifa ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF iliyowasilishwa katika kongamano hilo ambalo mwenyeji wake ni Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May imesema kuwa, raia milioni 2.9 wa Somalia wataendelea kuishi katika maeneo yanayokumbwa na ukame na baa la njaa hadi kufikia Juni mwaka huu, na hali hiyo inatazamiwa kuzidi kuwa mbaya iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa.
Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo ameliambia kongamano hilo kuwa, atafanya juu chini kuona anatekeleza yale yote aliyoyaahidi katika kampeni za uchaguzi wa rais, hususan kupambana na maadui watatu wakuu wa taifa hilo ambao ni ugaidi, njaa na ufisadi.
Genge la al-Shabaab linalovuruga usalama wa Somalia
Kongamano hilo linawaleta pamoja wadau wa kimataifa, Umoja wa Mataifa na nchi wafadhili ili kujaribu kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na kuiwezesha kufikia malengo yake ya maendeleo, usalama na kustawisha uchumi kufikia mwaka 2020.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages