Meya wa Tehran Mohammad Baqer Qalibaf amejiondoa katika mchuano wa kuwania urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika taarifa, Qalibaf amewataka wafuasi wake wamuunge mkono
Ibrahim Raisi, mgombea mwingine anayewania urais wa Iran. Amesema katika
taarifa hiyo: "Kwa ajili ya kuwepo umoja katika mrengo wa mapinduzi,
nimechukua uamuzi muhimu na wa kimsingi. Kwa ajili ya kulinda malengo
matukufu ninatoa wito kwa wafuasi wangu kote Iran kutumia uwezo wao wote
kuhakikisha Ibrahim Raisi Sadat anafanikiwa kuunda serikali ya 'Kazi na
Heshima' kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Mgombea mwingine ambaye ameripotiwa kujiondoa katika duru hii ya 12
ya uchaguzi wa rais wa Iran ni Mustafa Hashemi Taba ambaye Jumatatu
alitoa taarifa na kusema atampa kura yake rais wa sasa Hassan Rouhani.
Wagombea wengine wa urais ni Mostafa Aqa-Mirsalim ambaye ni waziri wa
zamani wa utamaduni na muongozo wa Kiislamu na Es'haq Jahangiri makamu
wa kwanza wa serikali ya sasa.
Uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa
kufanyika Ijumaa ya tarehe 19 mwezi huu wa Mei sambamba na uchaguzi wa
tano wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji kote nchini Iran.
Kamati ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema Wairani
zaidi ya milioni 56 wametimiza masharti ya kupiga kura na hivyo
wanatazamiwa kushiriki katika uchaguzi ujao wa urais.
Wairani wanaoishi nje ya nchi wataweza kupiga kura katika vituo 269
vya upigaji kura vilivyoko katika ofisi 131 za kidiplomasia za Jamhuri
ya Kiislamu ya Iran katika nchi 103 kote duniani.
No comments:
Post a Comment