Rais Donald Trump wa Marekani amemaliza safari yake ya mara ya kwanza barani Ulaya tangu aingie madarakani; bila ya kufikia natija iliyotarajiwa.
Katika duru ya safari hii, Trump alikutana na viongozi wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) mjini Brussels, Ubelgiji na kadhalika viongozi wa nchi wanachama wa kundi la G7 mjini Sicily, Italia. Kadhalika Trump kwa mara ya kwanza alifika Vatican na kukutana na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis ambapo pia alifanya naye mazungumzo. Katika vikao na mikutano hiyo kulijadiliwa masuala ya biashara, mabadiliko ya hali ya hewa, njia za kukabiliana na ugaidi na matokeo ya wimbi la wahajiri wanaoelekea barani Ulaya. Pamoja na hayo katika maudhui zote hizo kuliwabainikia walimwengu mpasuko wa mtazamo kati ya Marekani na waitifaki wake.
Katika suala la biashara, kundi la G7 kwa mara nyingine na kinyume na mtazamo wa Marekani, lilikosoa vikali sera za kiuchumi za Washington. Hata hivyo kundi hilo chini ya mashinikizo ya kamati ya Marekani kwa uongozi wa Trump mwenyewe, lilikubali katika kikao cha mjini Sicily, Italia kwamba vifungu vya ukosoaji wa kibiashara visivyo vya kiuadilifu, lazima viwekewe masharti maalumu. Kabla ya hapo viongozi wa Marekani walionyesha matumaini yao kwamba katika kikao cha kwanza cha viongozi wa kundi la G7 pamoja na Rais Donald Trump, muungano huo muhimu wa kiuchumi, ungeunga mkono sera za kiuchumi za Marekani.
Hata hivyo nchi kama vile Ujerumani, Japan, Ufaransa na Canada ambazo zinastawi katika uzalishaji na ambazo zimewekeza katika uzalishaji wa bidhaa kwenda masoko yenye watumiaji wengi ya Marekani, zilipinga madai ya kila siku ya Washington ya 'Marekani Kwanza.' Ama kuhusiana na suala la mabadiliko ya hali ya hewa pia viongozi wa kundi la G7 hawakuweza kufikia makubaliano na rais huyo wa Marekani. Hii ni kwa kuwa nchi za Ulaya za muungano huo zililipa kipaumbele suala la kuandaliwa na kutekelezwa mikataba ya kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, katika hali ambayo Trump aliahidi kuitoa nchi yake katika mkataba huo uliofikiwa mjini Paris, Ufaransa. Washirika wa Marekani katika kundi la G7 au katika Umoja wa Ulaya wana wasiwasi mkubwa endapo Marekani ambayo ndiyo nchi inayoharibu zaidi hali ya hewa duniani, itajitoa katika mkataba huo wa mjini Paris.
Inatabiriwa kuwa, tangazo la Washington la kujitoa katika mkataba huo, litatoa pigo jingine kwenye mahusiano yake na nchi za Ulaya na Asia. Mbali na kundi la G7, katika kikao na viongozi wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) mjini Brussels, Ubelgiji pia, Rais Donald Trump wa Marekani hakuweza kupata kile alichokuwa amekitarajia tangu awali. Kabla ya kikao hicho viongozi wa ngazi ya juu wa serikali ya Marekani walikuwa wametangaza kuwa, wana matumaini nchi wanachama katika muungano huo zitakubaliana na pendekezo la kuongezwa bajeti na kujiunga katika muungano wa eti kupambana na Daesh (ISIS). Kinyume kabisa na na matarajio ya Washington, hakuna kauli yoyote iliyotolewa katika kikao cha mjini Brussels, Ubelgiji ya kuunga mkono pendekezo hilo la Marekani.
Hii ni katika hali ambayo ilikuwa imepangwa baadhi ya nchi wanachama wa NATO ziongeze pesa zaidi za mchango kwa ajili ya masuala ya kiulinzi. Aidha katika suala la vita dhidi ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) nchi wanachama wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO), zilikubali tu kuunga mkono kilojestiki operesheni za muungano unaoongozwa na Marekani wa eti kupambana na Daesh. Hii ni katika hali NATO imetangaza rasmi kutoshiriki katika vita hivyo vya Daesh katika maeneo ya magharibi na kaskazini mwa Asia. Inaonekana wazi kuwa wasiwasi wa matokeo ya kiusalama na kisiasa katika vita vyao na kundi la Daesh, ndiyo sababu kuu ya nchi wanachama wa muungano huo wa kijeshi kutupilia mbali pendekezo la Marekani. Alaa kulli hal, msimamo wa miungano miwili ya NATO na kundi la G7 katika kupambana na ugaidi, imemfanya Donald Trump kushindwa kupata alichokitaka kutoka kwa washirika wake wakubwa. Inatazamiwa kuwa kushindwa huko kwa Washington kulikotokana na faili linalohusiana na uhusiano wa Trump na Russia kutaongeza mashinikizo ambayo hata hivi sasa si machache, dhidi ya serikali ya Marekani na Trump mwenyewe.
No comments:
Post a Comment