Katika hali ambayo baadhi ya duru za habari
zimearifu kupungua misimamo ya pande mbili kuhusiana na mgogoro wa
Peninsula ya Korea, yaani Marekani na Korea Kaskazini, Washington
imetuma meli yake ya kivita aina ya USS Ronald Reagan katika maji ya
karibu na Korea Kaskazini.
Kabla
ya hapo pia Marekani ilituma meli ya USS Carl Vinson kwenda katika maji
ya Peninsula ya Korea suala ambalo lilisababisha kuongezeka mvutano
katika eneo hilo. Korea Kaskazini iliitaja hatua ya kutumwa meli hiyo
katika maji ya eneo hilo kuwa ni sawa na kutangaza vita huku ikiionya
vikali Washington kutokana na madhara makubwa yanayoweza kutokea
kufuatia hatua hiyo ya kichokozi. Mbali na Pyongyang, Uchina pia
ilikutaja kupenda vita kwa Washington katika eneo hilo kuwa kunatokana
na siasa za kiuhasama za baharini ambapo ilimtaka Rais Donald Trump wa
Marekani kuachana na mwenendo huo.
Kwa kuzingatia indhari za mara kwa mara
za Korea Kaskazini juu ya utumwaji wa meli zaidi ya vita katika maji
yake, hivyo kitendo hicho cha Washington si cha kustaajabisha sana.
Kuhusiana na suala hilo kuna nukta kadhaa za kufaa kuashiriwa. Kwanza ni
kuwa, kutumwa meli zaidi za kivita za Marekani katika eneo kunabainisha
nafasi athirifu za kimtazamo na siasa za majenerali wa jeshi la nchi
hiyo kwa nafasi yao ya kimaamuzi katika ikulu ya nchi hiyo White House.
Hata hivyo suala hilo halihusiani tu na eneo pekee la Peninsula ya Korea
na mashariki mwa Asia, bali linashuhudiwa pia nchini
Afghanistan, Syria, Iraq na Yemen, ambapo makamanda wa jeshi la Marekani
wanahusika na kupanga ratiba za kuongeza majeshi ya nchi hiyo ndani ya
mataifa hayo.
Amma nukta ya pili ni kwamba, baadhi ya
wachambuzi wa mambo wameitaja hatua ya Marekani ya kutuma meli ya USS
Ronald Reagan katika maji ya Peninsula ya Korea kuwa yenye shabaha ya
mwisho ya Washington kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kufanya
mazungumzo na Pyongyang. Hii ni kusema kuwa hadi hivi sasa Pyongyang na
Washington zimejiandaa kufanya mazungumzo kwa masharti maalumu, hivyo
kitendo cha Marekani cha kuendelea kutuma zaidi meli zake za kivita
katika maji hayo ni aina fulani ya kuandaa mazingira kwa ajili ya
kuisukuma Korea Kaskazini kwenye meza ya mazungumzo. Pamoja na hayo
inaonekana kwamba, Moon Jae-in rais mpya wa Korea Kusini haoni kitendo
cha kutunishiana misuli baina ya Korea Kaskazini na Marekani kama
kinaweza kuandaa mazingira ya kufanyika mazungumzo ya pande mbili. Na ni
kwa ajili hiyo ndio maana akautaka Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na
Seoul, usaidie katika utatuzi wa mgogoro wa eneo la Peninsula ya Korea.
Katika mazungumzo ya simu na António
Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais Moon Jae-in wa Korea
Kusini, sambamba na kusisitizia suala hilo, alisema kuwa, kuhitimishwa
mgogoro wa eneo la Peninsula ya Korea kunahitajia ushirikiano wa Umoja
wa Mataifa na serikali ya Korea Kusini. Suala hilo linaonyesha kwamba,
serikali Seoul ambayo inahesabika kuwa muitifaki mkubwa wa Washington,
haikubaliani na siasa za Marekani kuhusiana na eneo hilo kama ambavyo
inazitambua siasa hizo kuwa ndizo zinazochafua usalama wa eneo hilo.
Marekani pia inafahamu vyema kwamba, mgogoro wa Peninsula ya Korea ikiwa
hautatatuliwa kwa njia za kisiasa na badala yake zikatumika njia za
kijeshi, basi utasababisha maafa makubwa. Hata kama kwa upande wa
usalama, Marekani inaonekana iko mbali na Peninsula ya Korea, lakini
kambi zake za kijeshi zilizoko Korea Kusini na Japan zitakuwa za kwanza
kuangamizwa na makombora ya Korea Kaskazini. Ni kwa ajili hiyo ndio
maana makamanda wa jeshi la Marekani hawapendelei kumaliza mgogoro wa
eneo hilo kwa njia za kijeshi.
Pamoja na hivyo, makamanda wa nchi hiyo
wanadai kuwa, kuongezeka mvutano wa eneo hilo kumeilazimisha Washington
kutuma zana za baharini katika maji ya eneo zikiwemo meli za kivita kwa
shabaha ya kufanya doria. Suala hilo lina maana kwamba, Marekani
inatumia mgogoro huo kwa ajili ya kuimarisha uwepo wake katika eneo hilo
kwa nia ya kuzidi kuizingira China. Wakati huo huo, naibu balozi wa
Korea Kaskazini katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, sasa umefika
wakati Marekani kuachana na siasa zake za uhasama dhidi ya Pyongyang.
Kim In Ryong amesema kuwa, kabla ya Marekani kuanza mazungumzo yoyote na
Korea Kaskazini, kwanza inatakiwa kuachana na siasa zake za uadui dhidi
ya nchi yake.
No comments:
Post a Comment