Tuesday, May 23, 2017

RAIS ROUHANI AFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS MPYA WA UFARANSA

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran itaendelea kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya Vienna.
Rais Rouhani aliyasema hayo jana jioni katika mazungumzo yake ya simu na Rais mpya wa Ufaransa, Emmanuel Macron na kusisitiza kuwa, Iran itatekeleza wajibu wake wa kimataifa kwa kutekelezwa ipasavyo makubaliano hayo yanayofahamika kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Aidha ameitaka Ufansa na Umoja wa Ulaya kwa ujumla kutekeleza barabara makubaliano hayo ya JCPOA. Kadhalika Dakta Rouhani amesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano na ushirikiano wa kibiashara wa pande mbili kati ya Iran na Ufaransa katika  nyuga mbalimbali ikiwemo miundombinu na sekta ya uchukuzi.
Kwa upande wake, Macron amempongeza Rais Hassan Rouhani kwa kuchaguliwa tena kuongoza muhula wa pili, baada ya kushinda katika uchaguzi wa rais uliofanyika hivi karibuni hapa nchini.
Viongozi walioshiriki kusainiwa JCPOA mjini Vienna Julai 14, 2015
Kadhalika rais huyo mpya wa Ufanasa amesisitiza kuwa, JCPOA ni makubaliano muhimu ambayo yakitekelezwa ipasavyo na pande zote, yatatoa mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa eneo na kimataifa.
Aidha amesema Paris iko tayari kushirikiana na Tehran katika nyuga za uchumi, benki, utamaduni, utalii na elimu.
Ikumbukwe kuwa, tarehe 14 Julai 2015, Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 ambazo ni Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Marekani na Ujerumani zilisaini mkataba kuhusiana na shughuli za nyuklia za Iran ambao utekelezaji wake ulianza Januari 16 mwaka uliopita wa 2016.

No comments:

Post a Comment