Serikali ya Korea Kaskazini imetangaza kuwa,
kombora la balestiki ililolifanyia majaribio siku ya Jumapili iliyopita,
inaweza kubeba kichwa cha nyuklia nzito.
Katika jaribio hilo lilisimamiwa
na Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini. Picha zilizorushwa na
vyombo vya habari vya nchi hiyo zilimuonyesha kiongozi huyo akifuatilia
kwa karibu shughuli za urushaji wa kombora hilo. Katika picha zingine,
kiongozi huyo alionekana akiwa na makamanda wa jeshi akipiga makofi kwa
kuonyesha mafanikio ya jaribio hilo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi sasa Pyongyang imewekewa
vikwazo mbalimbali na Umoja wa Mataifa kutokana na miradi yake ya silaha
za nyuklia. Kufuatia jaribio hilo, Rais Donald Trump wa Marekani
alitishia kuiwekea vikwazo vikali zaidi Korea Kaskazini, baada ya
Pyongyang kufyatua kifaa kinachoaminika kuwa kombora hilo la balestiki
kuelekea upande wa Japan. Taarifa ya Ikulu ya Marekani ya White House
ilisema kuwa, uchokozi mpya wa Korea Kaskazini unafaa kuwa kengele ya
hatari kwa nchi zote duniani, na kwamba jamii ya kimataifa inafaa
kutekeleza vikwazo vikali zaidi kwa nchi hiyo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Marekani yenyewe imekuwa ikifanya
majaribio kadhaa ya silaha za nyuklia, mbele ya kimya cha jamii ya
kimataifa. Korea Kaskazini imekuwa ikisisitiza kuwa itaendelea
kujiimarisha kwa silaha hizo na makombora ya balestiki ili kujiandaa na
vitisho na harakati za kijeshi za Marekani na washirika wake katika eneo
la Peninsula ya Korea. Katika hatua nyingine, serikali ya Washington na
Seoul, zimefikia makubaliano yenye lengo la kuiwekea mashinikizo Korea
Kaskazini kutokana na silaha zake hizo hatari.
No comments:
Post a Comment