Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, imeongeza muda wa kupiga kura katika uchaguzi wa duru ya 12 ya urais.
Taarifa iliyotolewa na Tume cha
Uchaguzi jioni ya leo imesema kuwa muda wa kupiga kura umeongezwa hadi
saa 4:00 za usiku kwa upande wa Tehran na kwa upande wa vijijini
ukiongezwa hadi saa 3:00 za usiku. Imeongeza kuwa, imeamua kuongeza muda
huo kutokana na mapendekezo yaliyowasilishwa kutoka vituo vya kupigia
kura juu ya kuongezwa muda na baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani kutaka
kuongezwa muda wa saa mbili wa shughuli hiyo.
Tume ya Uchaguzi ya Iran pia imeongeza
muda wa saa moja wa upigaji kura wa uchaguzi wa duru ya tano ya mabaraza
ya miji na vijiji. Ushiriki mkubwa wa hamasa wa wananchi wa Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran, unatajwa kuwa sababu ya kuongezwa muda huo. Hadi
tunaingia studioni, shughuli ya upigaji kura bado ilikuwa inaendelea,
ambapo vituo vya kupigia kura vimeonekana kufurika kwa wingi wananchi
muda wote.
Wakati huo huo, katibu mkuu wa Umoja wa
Waashuri Duniani, amesema kuwa ushiriki mkubwa wa wananchi wa Iran
kutoka watu wa kila kaumu, matabaka na dini mbalimbali katika uchaguzi
wa rais wa leo, ni suala lililowashangaza wengi. Yonatan Bet Kolya,
ameyasema leo katika mazungumzo na Shirika la Habari la IRNA na
kuongeza kuwa, umoja ulioonyeshwa na taifa la Iran katika ushiriki
mkubwa wa watu kwenye upigaji kura ni suala lililowashangaza wengi
duniani.
No comments:
Post a Comment