Vituo vya kupigia kura tayari vimeshafunguliwa nchini
Iran na raia wa nchi hiyo wanachagua rais wao mpya. Lakini ni nani
wagombea wakuu wanaopigania nafasi ya urais katika uchaguzi wa leo?
Kuchaguliwa tena au kutochaguliwa kwa rais wa sasa Hassan Rouhani
kunaweza kuwa na athari kubwa kwa siasa sio tu za ndani ya Jamhuri hiyo
ya Kiislamu, bali pia kimataifa, kwani uchaguzi huu unaweza kwa kiasi
kikubwa kuathiri mustakbali wa baadaye wa nchi hiyo.
Takriban
vituo vya kupigia kura 63,000 vimefunguliwa leo hii kuanzia saa mbili
asubuhi, nchini kote. Hata hivyo, kutokana na kuwepo watu milioni 54
walio na haki ya kupiga kura, pamoja na kuwepo kawaida ya wananchi
kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupiga kura, matokeo ya awali
hayatarajiwi kutolewa hadi Jumamosi.
Uwezo wa Iran wa silaha za
kinyuklia na umuhimu wa kimkakati ulio nao nchi hiyo katika eneo la
Ghuba na Mashariki ya Kati, ni masuala mawili makuu yanayozingatiwa
wakati wa kupiga kura leo hii.
Wapiga kura nchini humo wataweza kuchagua miongoni mwa wagombea wanne.
Rais aliyepo madarakani Hassan Rouhani
Kwanza
ni Hassan Rouhani msomi wa kidini na mwanasheria mwenye umri wa miaka
68 na ndiye rais aliyepo madarakani kwa sasa. Rouhani anatazamwa kama
mwanamageuzi wa misimamo ya wastani, na ni mmoja wa wagombea wawili
wanaongoza katika kinyang'anyiro hicho cha urais akifuatiwa na Ebrahim
Raisi.
Wakati wa muhula wake wa kwanza Rouhani, alifungua milango
ya nchi hiyo na kuzikaribisha nchi za Magharibi, alisimamia makubaliano
ya 2015 ambayo yaliihitaji Iran kupunguza uwezo wake wa kinyuklia, ili
nchi za Magharibi kwa upande wake zipunguze vikwazo vya kimataifa
ilivyoiwekea nchi hiyo. Rouhani ameahidi kuendeleza mahusiano ya
kidiplomasia na amesema ataendelea na kazi ya kuvutia zaidi uwekezaji wa
kimataifa nchini Iran iwapo atachaguliwa tena.
Mgombea urais wa Iran Ebrahim Raisi
Mgombea
wa pili ni Ebrahim Raisi, kiongozi wa kidini mwenye umri wa miaka 57
ambaye anatazamwa kama mshirika wa karibu na anayeweza kumpokea madaraka
Kiongozi Mkuu wa Kidini, Ali Khamenei.
Ingawa Raisi hataki
kusitisha makubaliano ya kinyuklia yaliyofikiwa mwaka 2015, lakini
amesema Iran inapaswa kujitenga kisiasa na kiuchumi kutoka nchi za
Magharibi. Raisi pia anapinga uwekezaji zaidi wa kigeni.
Mgombea urais katika uchaguzi wa Iran Mostafa Mirsalim
Mostafa
Mirsalim ni mgombea mwengine wa tatu ambaye aliwahi kuwa waziri wa
utamaduni na anatazamwa kama mtu mwenye misimamo mikali ya kihafidhina.
Nafasi yake ya kushinda katika uchaguzi huu inatarajiwa kuwa ni ndogo
sana.
Na mgombea wa nne katika uchaguzi wa leo wa rais
unaofanyika nchini Iran ni Mostafa Hashemitaba. Mgombea huyo mwenye umri
wa miaka 76 na mwenye misiamamo ya kisiasa ya wastani aliwahi kuwa
makamu wa rais kuanzia 1997 - 2005 chini ya uongozi wa Mohammad Khatami,
mwanamageuzi wa kwanza kuwahi kuwa rais nchini humo.
Mgombea urais wa Iran Mostafa Hashemitaba
Uhusiano
mzuri wa kidiplomasia kati ya Iran na nchi za Magharibi kama vile
Marekani pamoja na nchi jirani Saudi Arabia, ambayo ni msaidizi muhimu
wa makundi ya waasi ya nchini Syria, unaweza kurahisisha mazungumzo ya
amani siku za baadaye.
No comments:
Post a Comment