Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania
amekataa ombi la marais wa Tanzania na Uganda la kuutaka umoja huo
uifutie vikwazo Burundi.
Roeland van de Geer amenukuliwa na
mtandao wa habari wa Africa Times akitoa msimamo huo wa Umoja wa Ulaya
baada ya marais wa Tanzania na Uganda kutaka kuondolewa vikwazo Burundi
na kusema kuwa vikwazo hivyo vitaendelea hadi hali ya kisiasa
itakapobadilika nchini humo.
Ikumbukwe kuwa katika mkutano wa
kukabidhiana uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC uliofanyika
jijini Dar es Salaam Tanzania siku ya Jumamosi, Rais Yoweri Museveni wa
Uganda na mwenzake wa Tanzania, John Pombe Magufuli waliutaka Umoja wa
Ulaya ufute vikwazo ulivyoiwekea Burundi.
Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Yoweri Museveni
wa Uganda alisema kuwa, jumuiya hiyo inapinga uamuzi wa Umoja wa Ulaya
wa kumuwekea vikwazo mwanachama wa jumuiya hiyo.
Mgogoro mkubwa wa kisiasa umeikumbwa
Burundi tangu Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo alipoamua kugombea
tena urais kwa mara ya tatu mfululizo huku wapinzani wakisema kuwa huo
ulikuwa ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya Arusha, Tanzania,
yaliyomaliza vita vya ndani nchini Burundi.
Uchaguzi mkuu wa Burundi ulisusiwa na
wapinzani, na Umoja wa Ulaya nao ukaiwekea vikwazo nchi hiyo. Mgogoro
huo umesababisha matatizo mengi yakiwemo mauaji na wimbi kubwa la
wakimbizi wa ndani na nje ya Burundi.
No comments:
Post a Comment