Rais wa Marekani Donald Trump anasafiri kuelekea Ghuba
katika ziara yake ya kwanza kabisa ya nje ya nchi tangu achukue hatamu
za uongozi.
Tangu Rais Jimmy Carter, Trump ndiye rais wa kwanza kufanya ziara yake ya kwanza mbali na nchi za karibu kama Mexico na Canada.
Anaanza kwa kuizuru Saudi Arabia, eneo lililo mbali kabisa na matatizo
mengi ya nyumbani. Ziara hiyo ya rais wa Marekani huko Saudi Arabia
itashuhudia kutiwa saini mkataba wa dola bilioni 100 wa silaha baina ya
nchi hizo mbili.
Elliot Abraham ni afisa kutoka baraza lenye
ushawishi mkubwa la masuala ya nchi za nje, "ni jambo la kuridhisha, kwa
sababu wakati wa kampeni za uchaguzi, Donald Trump alizungumzia
kuhusiana na Marekani kujiondoa kutoka kwenye mizozo yote ya Mashariki
ya Kati," alisema Elliot, "na sasa ziara yake ya kwanza ya nje ya nchi
inashuhudia yeye kuelekea huko huko Mashariki ya Kati."
Viongozi wa Kiarabu walikuwa na matumaini na urais wa Trump
Ikulu
ya White House ilisema kwamba Trump anasafiri ili kuuleta pamoja
ulimwengu wa Kiislamu dhidi ya maadui. Atakutana na mfalme Salman ibn
Abd al-Aziz pamoja na wengine katika familia hiyo ya kifalme na
ahudhurie pia mkutano wa mataifa ya Kiarabu. Trump pia atatoa hotuba ya
kukashif masuala ya itikadi kali katika mkutano wake na viongozi wa
karibu mataifa 50 ya Kiarabu na Kiislamu. Marais wa mataifa hayo
walipewa mwaliko maalum mjini Riyadh ili wakutane na rais huyo wa
Marekani.
Trump atakutana na mfalme wa Saudi Arabia Salman Bin Abdul Aziz
Nile
Gardiner kutoka Wakfu wa Urithi wa Kihafidhina, unaoishauri serikali ya
Marekani kuhusiana na masuala muhimu ya nchi za kigeni na ndani ya nchi
anasema, viongozi katika mataifa ya Kiarabu walikuwa na matumaini
makubwa kuhusiana na urais wa Trump licha ya matamshi yake ya kukashif
Uislamu wakati wa kampeni na zile juhudi zake za kuweka marufuku ya muda
ya mataifa saba ya Waislamu kuingia nchini humo.
"Lengo la ziara
hiyo ni kuufufua uhusiano baina ya Marekani na Saudi Arabia na
kuwahakikishia Wasaudi Arabia kwamba Marekani iko tayari kutilia kikomo
ushawishi wa Iran unaoleta msukosuko katika eneo hilo," alisema
Gardiner.
Uhusiano wa Trump na Saudi Arabia utakuwa mtulivu
Gardiner
anazidi kusema kwamba, rais wa zamani Barack Obama alizipuuza nchi
marafiki wa Marekani katika eneo hilo la Mashariki ya Kati.
Barack Obama anashutumiwa na Warepublican kwa kuuharibu uhusiano wa Marekani na Saudi Arabia
Emma
Ashford kutoka taasisi ya libertarian Cato, anasema "Uhusiano wa Trump
na Saudi Arabia utakua mtulivu kuliko ulivyokuwa wakati wa Obama, lakini
hili halitoi hakikisho kwamba ni jambo zuri kwa sera ya nchi za nje ya
Marekani."
Huko Riyadh kinyume na mtangulizi wake bwana Obama
alivyofanya mjini Cairo mwaka 2009, Trump hatoielekeza hotuba yake kwa
raia wa Kiarabu bali viongozi wao, isitoshe, masuala ya kukiukwa kwa
haki za kibinadamu yatajadiliwa faraghani na hii ndiyo inayoonekana kuwa
sera ya kigeni ya Trump.
No comments:
Post a Comment