Mlipuko huo ulitokea baada ya tamasha la muziki katika ukumbi wa Manchester Arena Jumatatu (22.05.2017) usiku. Mlipuko ulitokea wakati watu walipokuwa wakiondoka baada ya tamasha kukamilika.
Polisi nchini Uingereza wanasema watu wasiopungua 22 wameuawa na wengine 59 kujeruhiwa kwenye mlipuko uliotokea mwishoni mwa tamasha la muziki la mwanamuziki wa Marekani Ariana Grande mjini Manchester kaskazini magharibi mwa England. Watoto ni miongoni mwa waliouawa katika shambulizi hilo la kigaidi linaloulizwa kuwa baya kabisa katika kipindi cha miaka 12. Maafisa wawili wa Marekani wamesema mshambuliaji wa kujitoa muhanga anashukiwa kuhusika na mlipuko huo.
Mashabiki waliokuwa wakipiga mayowe, wengi wao vijana wanarika, walikimbia kutoka eneo la tukio wakiwa na hofu baada ya mlipuko huo wa bomu baada ya tamasha kukamilika."Nilihisi moto katik shingo yangu na nilipotazama nikaona maiti kila mahala," alisema Elena Semino, aliyekuwa akimtafuta mtoto wake wa kike wa umri wa miaka 17, alipozungumza na gazeti la Guardian.
Semino, ambaye mwenyewe alijeruhiwa, alisema alikuwa amesimama kando ya ofisi ya kutoa tiketi ya ukumbi wa Manchester Arena wenye nafasi za watu 21,000 wakati mlipuko ulipotokea.
"Mlipuko mkubwa kama wa bomu ulitokea ambao ulimfanya kila mtu kujawa na taharuki na sote tulikuwa tunajaribu kukimbia kutoka ukumbini," alisema Majid Khan, mwenye umri wa miaka 22 ambaye alikuwa katika tamasha hilo na dada yake.
Magari ya kubebea wagonjwa na timu za wataalamu wa kutengua mabomu walikimbi katika eneo hilo huku jamaa wa familia wakiwatafuta wapendwa wao na wakazi wakifungua milango ya nyumba zao kuwakaribisha watu waliokuwa wamehudhuria tamasha hilo baada ya safari za treni kufutwa.
"Watoto ni miongoni mwa watu 22 waliouliwa katika shambulizi hilo, huku watu 59 wakijeruhiwa," alisema Ian Hopkins, Mkuu wa jeshi la polisi Geater Manchester, mapema siku ya Jumanne.
Kampeni za siasa zasitishwa
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amelaani vikali shambulizi hilo la kinyama na kusitisha kamepni yake kuelekea uchaguzi mkuu Juni 8 kama alivyofanya kiongozi mkuu wa upinzani, Jeremy Corbyn. "Tunawakumbuka wahanga na kuziombea dua familia za wote walioathiriwa," alisema Bi May, ambaye anatarajiwa kuongoza kikao cha dharura cha kamati ya usalama kuanzia saa tatu asubuhi.
"Tunafanya juhudi kupata taarifa kamili kuhusu kile kinachochukuliwa na polisi kuwa shambulizi la kigaidi," alisema May katika taarifa.
Rais wa China Xi Jinping alituma risala zake za rambirambi kwa Malkia Elizabeht wa Uingereza kuhusu mlipuko wa mjini Manchester.
Polisi wa Manchester wanasema wanashirikiana na polisi ya taifa na mashirika ya kijasusi kuchunguza mlipuko huo. Meya wa mji wa London Sadiq Khan ametuma risala zake za rambirambi kwa jamii za wahanga na amesema mji wa London unasimama pamoja na mji wa Manchester kufuatilia tukio hilo.
No comments:
Post a Comment