Mgombea urais mwenye siasa kali za mrengo wa kulia
nchini Ufaransa, Marine Le Pen, na hasimu wake Emmanuel Macron
anayefuata siasa za mrengo wa kati wamekutana kwenye mdahalo uliogubikwa
na kukashifiana waziwazi.
Kama ilivyokuwa imetazamiwa kabla, mdahalo huo uliorushwa moja kwa
moja kwenye televisheni ulikuwa wa piga-nikupige, kila mmoja akitumia
maneno makali kadiri alivyoweza kuishusha hadhi ya mwengine mbele ya
wapigakura wao, na pia akijidhihirisha alivyo na msimamo tafauti
takribani kwenye kila jambo.
Ambapo Emmanuel Macron alijikita
kwenye kunadi sera zake za uwazi na mageuzi ya soko, Le Pen alihamia
zaidi kwenye msimamo wake wa uzalendo kwa Ufaransa. Tangu katika dakika
ya mwanzo ya mdahalo huo, Le Pen alimpachika majina Macron akimuita
"mgombea wa tabaka la wachache" na "kipenzi cha mfumo".
Majibu
ya Macron dhidi ya tuhuma hizo, yalikuwa ni Le Pen, ambaye ni kizazi cha
uongozi wa chama cha National Front, ndiye "mrithi wa mfumo ambao
umeneemeka kutokana na majanga ya watu wa Ufaransa kwa miongo kadhaa",
akiongeza kuwa Le Pen anacheza na hisia za khofu walizonazo watu ili
kuvuna kura zao.
"Wewe hujali kuhusu nchi hii, huna mpango wowote
nayo. Mpango wako ni kuwaambia Wafaransa mtu huyu ni mbaya, kuwachafua
watu, kuongoza kampeni ya uongo na uzushi. Mpango wako ni kuwafanya watu
waishi kwa khofu na uongo. Ndicho chakula chako. Ndicho chakula cha
baba yako kwa miongo kadhaa, chakula cha Wafaransa wa mrengo mkali wa
kulia na ndicho kilichokutengeneza wewe," alisema Macron.
Le Pen asema Ufaransa lazima itawaliwe na mwanamke
Mabango ya wagombea wa duru ya pili ya uchaguzi wa rais nchini Ufaransa siku nne kabla ya kura ya tarehe 7 Mei 2017.
Kuhusu
sera zao kuelekea bara la Ulaya, Le Pen alimtuhumu Macron kuwa myonge
mbele ya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, akidhihaki kwamba Ufaransa
lazima itaongozwa tu na mwanamke, ama awe yeye, Le Pen, au Kansela
Merkel.
"Ukweli ni kwamba ulikwenda kumuona Bi Merkel kumuomba
baraka zake. Kwa sababu huwezi kufikiria kufanya jambo lolote bila ya
ruhusa ya Bi Merkel. Ndio maana ulipoulizwa vipi utakabiliana na Merkel,
ulisema hutokabiliana naye, bali utakuwa pamoja naye."
Wagombea
wawili hao walionesha tafauti zao pia kuelekea uundikaji wa jamii ya
Kifaransa, ambapo Macron alielezea Ufaransa ya mchanganyiko kama ilivyo,
huku Le Pen akimtuhumu kuwa legelege sana dhidi ya Waislamu wenye siasa
kali.
Uchunguzi wa maoni uliofanywa na kampuni ya Elabe na
kuchapishwa muda mfupi baada ya mdhalo huo, ulionesha kuwa asilimia 63
ya watu walimuona Macron kuwa amewashawishi zaidi dhidi ya asilimia 34
za Le Pen.
Maoni ya jumla yanaonesha kuwa Macron atashinda kwa
asilimia 59 dhidi ya 41 za Le Pen ikiwa uchaguzi utafanyika sasa, lakini
midahalo kama hii ya lala salama huko nyuma imekuwa ikibadili muelekeo
wa mambo.
No comments:
Post a Comment