Umoja wa Mataifa umesema watu zaidi ya
milioni 31 walilazimika kuwa wakimbizi ndani ya nchi zao mwaka uliopita
wa 2016 lote duniani.
Ripoti ya UN imesema kuwa, idadi kubwa ya wakimbizi hao wa
ndani ya nchi ilisajiliwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na
Syria, kutokana na kushadidi migogoro na majanga ya kimaumbile.
Jan Egeland, Mkuu wa Baraza la Wakimbizi la Norway amesema mwaka
uliopita, kwa kila sekunde, mtu mmoja alilazimika kuhama makazi yake
kutokana na migogoro, mapigano na majanga ya kimaumbile kama mafuriko,
maporomoko ya ardhi na mikasa ya moto.
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, watu 922,000
walifurushwa makwao mwaka jana 2016 huko Kongo DR, 824,000 nchini Syria,
Wairaqi 659,000, Waafghani 653,000 huku watu 501,000 wakilazimika kuwa
wakimbizi wa ndani nchini Nigeria.
Mwezi uliopita, Yvon Edoumou, afisa katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa
ya Masuala ya Kibinadamu (OCHA) alisema kuwa, ofisi hiyo imesajili
wakimbizi wa ndani milioni 1.09 katika mkoa wa Kasai, katikati mwa Kongo
kuanzia Aprili Mosi mwaka huu.
No comments:
Post a Comment