Duru ya nne ya mazungumzo ya mjini Astana,
Kazakhstan ilianza Jumatano ya jana. Duru hiyo ya mazungumzo ya Syria
imefanyika huku yakishuhudiwa mabadiliko madogo kwa upande wa washiriki.
Jumbe za makundi ya wapinzani wa
Syria zinazoshiriki mazungumzo hayo, takribani ni zile zile
zilizoshiriki mazungumzo yaliyopita. Ujumbe unaoiwakilisha serikali ya
Damascus, unaongozwa na Bashar Jaafari, mwakilishi wa nchi hiyo katika
Umoja wa Mataifa, huku timu ya Umoja wa Mataifa ikiwakilishwa na Staffan
de Mistura, mjumbe wa Katibu Mkuu wa umoja huo nchini Syria. Katika
muundo wa jumbe za Iran, Russia na Uturuki ambazo ni watazamaji wa
mazungumzo hayo, nazo hazijashuhudia mabadiliko yoyote. Mabadiliko
muhimu yaliyoshuhudiwa yalikuwa ya mwakilishi wa Marekani 'Stuart Jones'
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo katika masuala ya Mashariki
ya Kati, ambaye amechukua nafasi ya balozi wa nchi hiyo huko Kazakhstan
katika kikao hicho.
Duru hiyo ya mazungumzo ikilinganishwa
na duru ya tatu ya mazungumzo ya Astana nayo pia ingali inakabiliwa na
vikwazo vingi. Matatizo muhimu katika mazungumzo ya Astana Nne
yanatokana na hatua za kijeshi za mashambulizi ya Marekani ya tarehe
saba Aprili dhidi ya kambi ya jeshi la anga ya Syria katika mji
wa Shayrat, mkoani Homs na kadhalika mashambulizi tofauti ya Israel
katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo. Hatua hizo za kijeshi ndizo
zimepelekea hata kukosekana matumaini kuhusiana na mazungumzo ya Syria.
Hii ni katika hali ambayo katika duru ya mwisho ya mazungumzo ya mjini
Astana na Geneva ambazo zilifanyika mwezi Machi mwaka huu, kulikuwepo na
matarajio mengi kuhusiana na njia za utatuzi wa kisiasa kuhusiana
na mgogoro wa Syria, kiasi kwamba kwa mara ya kwanza katika duru ya
mwisho ya mazungumzo ya Geneva, timu za wapinzani na ile ya upande wa
serikali ya Damascus, zilifanya mazungumzo ya ana kwa ana baina yao.
Kizuizi kingine katika mazungumzo ya
Astana Nne, ni miamala ya kujikariri ya wapinzani wa serikali ya Syria.
Hii ni kusema kuwa, katika kikao hicho wapinzani wa serikali kama
ilivyokuwa katika kikao cha duru ya tatu, wamefanya ukwamishaji mwingi
wa mambo. Hii ni katika hali ambayo kwa mujibu wa baadhi ya habari
wapinzani wa Syria jana waliahirisha kushiriki mazungumzo hayo na badala
yake wameamua kujiunga na meza ya mazungumzo hayo leo, huku baadhi ya
duru zikisema kuwa, awali wapinzani hao walishiriki kwenye meza ya
mazungumzo na kuondoka kwenye mazungumzo hayo baadaye. Inaelezwa kuwa,
tangu mapema wapinzani hao walitangaza kuwa wasingeshiriki
mazungumzo hadi pale mashambulizi ya anga ya jeshi la serikali dhidi
maeneo wanayoyadhibiti huko Syria yatakapositishwa.
Inaonekana kuwa, ukwamishaji huo
unasababishwa na kutoweka matumaini yao juu ya kufikiwa malengo ya
kuidhoofisha serikali ya Damascus katika mashambulizi ya Marekani
ya tarehe saba Aprili dhidi ya kambi ya jeshi la anga ya Syria katika
mji wa Shayrat, mkoani Homs na pia hujuma kama hizo za Israel katika
maeneo tofauti ya nchi hiyo. Tunaweza kusema kuwa, mazungumzo ya Astana
Nne yamefeli hata kabla ya kuanza kwake, kutokana na miamala hasi ya
serikali ya sasa ya Marekani katika kipindi cha miezi miwili ya hivi
karibuni. Pamoja na hayo lazima tukubali kwamba mazungumzo ndio njia
muhimu kwa ajili ya utatuzi wa mgogoro wa Syria.
Kama ambavyo kuendelea mazungumzo hayo, kunaweza kupunguza taathira
ya mashambulizi ya kijeshi ya Marekani ya mwezi Aprili dhidi ya Syria na
kufufua matarajio kwa ajili ya kufikiwa makubaliano kuhusiana na
mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu.
No comments:
Post a Comment