Gazeti la The Independent linalochapishwa
Uingereza limemuelezea Rais wa Marekani na Waziri wa Ulinzi wa Saudi
Arabia kuwa ni watu hatari zaidi duniani.
Makala iliyoandikwa kwenye toleo la siku ya Jumamosi la gazeti
hilo imeashiria safari itakayofanywa siku chache zijazo na Rais Donald
Trump wa Marekani nchini Saudia na kuandika kuwa Trump ameiahidi Saudia
msaada mkubwa kwa operesheni za kijeshi za Riyadh nchini Yemen; na hivi
sasa kaimu mrithi wa ufalme ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi wa Saudia
Muhammad bin Salman anafanya juu chini kuishawishi Washington iiunge
mkono nchi hiyo katika kukabiliana na Iran.
Katika makala hiyo ya gazeti la Independent imeelezwa kuwa Marekani
na Saudi Arabia zimekubaliana kushadidisha misimamo yao dhidi ya Iran;
na uamuzi wa kwanza ziliouchukua ni kuziunga mkono jamii za wachache
nchini Iran zijitenge na mfumo wa Iran, ambapo ripoti za awali
zilizotolewa zinahusu mipango ya pamoja ya Washington na Riyadh ya
kuwaunga mkono Mabaluchi wa kusini mashariki mwa Iran.
Ripoti hiyo kupitia makala ya gazeti la The Independent imetolewa
katika hali ambayo mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
katika Umoja wa Mataifa Gholam-Ali Khoshrou, yapata siku kumi zilizopita
alimwandikia barua ya malalamiko Katibu Mkuu na Rais wa Baraza la
Usalama la umoja huo akieleza kwamba matamshi yaliyotolewa na Muhammad
bin Salman dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu alipotamka kwamba "lengo la
Saudia ni kuvihamishia vita ndani ya mipaka ya Iran" ni utoaji vitisho
wa wazi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ni ukiukaji wa kipengele
cha nne cha kifungu cha pili cha Hati ya Umoja wa Mataifa.
Khoshrou alisisitiza kwamba matamshi ya kihasama na kiadui ya Waziri
wa Ulinzi wa Saudia si ya utoaji vitisho tu dhidi ya Iran lakini pia
yana maana ya kukiri waziwazi utawala wa Aal Saud kwamba unahusika na
vitendo vya kigaidi na machafuko vinavyofanywa ndani ya ardhi ya Iran,
ambapo kuuliwa shahidi walinzi tisa wa mpakani wa Iran na genge la
wahalifu wanaoungwa mkono na kusaidiwa kifedha na Saudia ni mfano wa
karibuni kabisa wa suala hilo.
Hoja kwamba siasa za Saudia ni hatari ilishathibitishwa tokea hapo
kabla. Kwa hatua zake mbalimbali, Saudi Arabia ilisababisha kuundwa
makundi ya kigaidi ya Al-Qaeda na Taliban katika muongo wa 1990 na
kuanzia mwaka 2003 ikaunga mkono vitendo vya kigaidi na vya kuvuruga
utulivu na uthabiti ndani ya Iraq na kupelekea kuundwa Daesh,
Jabhatu-Nusra na makundi mengine ya kigaidi katika ardhi ya nchi hiyo
pamoja na Syria.
Kutokana na mtazamo wa fikra mbovu na potofu ilionao serikali mpya ya
Marekani, hivi sasa hatua hizo haribifu za Saudia zimegeuka kuwa fursa
kwa utawala wa Aal Saud ya kujionyesha na kuhalalisha sera zake za
hujuma na uvamizi dhidi ya nchi za eneo.
Serikali ya Marekani, hasa baada ya kuingia madarakani Donald Trump,
imechukua maamuzi yasiyo ya kiutu na kukanyaga usuli na misingi ya hisia
za ubinadamu na Hati ya sheria za kimataifa. Mfano hai wa maamuzi hayo
ni kuziuzia silaha zilizopigwa marufuku tawala zinazosifika kwa mauaji
ya watoto kama Saudia na Israel.
Ushirikiano huo hatari sasa unaonekana kuingia kwenye awamu mpya kwa
safari inayokaribia kufanywa na Trump nchini Saudi Arabia. Athari za
mshikamano huo uliopo baina ya Riyadh na Washington zimezidi kudhihirika
kwa hatua ya Marekani ya kubariki mauzo ya silaha zenye thamani ya
mabilioni ya dola kwa Saudia na kuwepo ukuruba mkubwa zaidi wa uhusiano
kati ya Aal Saud na utawala wa Kizayuni wa Israel, sambamba na kushadidi
mbinyo na mashinikizo dhidi ya muqawama wa Kiislamu katika eneo la
Mashariki ya Kati. Mwenendo huu umezifanya duru nyingi za kisiasa na za
wachambuzi wa masuala ya eneo kufuatilia kwa karibu malengo ya safari
inayokaribia kufanywa na Trump huku zikiwa na wasiwasi mkubwa wa maamuzi
hatari yanayoweza kuchukuliwa na Marekani na Saudia. Sababu ni kwamba
siasa za Washington na Riyadh hazina muelekeo wowote wa kuleta amani na
usalama katika eneo hili.../
No comments:
Post a Comment