Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan amesema mashambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni katika nchi jirani ya Misri sawa na hujuma nyingine za kigaidi katika sehemu mbali mbali duniani hazina uhusiano wala mafungamano yoyote na dini ya Kiislamu.
Akihutubu hapo jana katika dhifa ya futari iliyoandaliwa na Wakristo wa Kikhufti mjini Khartoum, Bashir sambamba na kulaani hujuma za hivi karibuni dhidi ya Wakristo nchini Misri amesema harakati za kigaidi popote pale hazina ufahamu wowote kuhusu dini ya wanadamu.
Rais wa Sudan amenukuliwa na shirika rasmi la habari la nchi hiyo SUNA akisema kuwa, mashambulizi hayo hayakuwa dhidi ya Wakristo wa Kikhufti tu, bali jamii yote ya Wamisri huku akitoa salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa hujuma hizo.
Ijumaa iliyopita, watu wasiopungua 28 waliuawa nchini Misri na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia shambulio la kigaidi dhidi ya mabasi mawili yaliyokuwa yamewabeba Wakristo wa Kibti kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo Cairo.
Kadhalika mwezi Aprili mwaka huu miripuko ya kigaidi katika makanisa mawili ya mji wa Tanta katikati ya mkoa wa al-Gharbiyah na mjini Alexandria nchini humo yalisababisha watu karibu 50 kuuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa.
Mashambulizi mengi ya kigaidi ya miaka ya hivi karibuni nchini Misri yamekuwa yakifanywa na kundi la Ansar Bait al-Muqaddas lililotangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi la Daesh, na kisha kubadilisha jina na kujiita Wilaya ya Sinai.
No comments:
Post a Comment