Idara ya upelelezi ya Ujerimani BfV imeripoti
kuongezeka kwa ujasusi wa Uturuki nchini Ujerumani, huku waziri wa mambo
ya nje wa Uturuki akiitaka serikali mjini Berlin kuamua iwapo Ujerumani
ni rafiki wa Uturuki au la.
Idara ya uchunguzi wa ndani ya Ujerumani ya BfV, imesema mgawanyiko
nchini Uturuki kuelekea kura ya maoni ya tarehe 16 Aprili kuhusu
kuimarisha madaraka ya rais Recep Tayyip Erdogan imejitokeza nchini
Ujerumani. BfV imesema katika taarifa kuwa inafautilia kwa karibu
ongezeko kubwa katika juhudi za ujasusi wa Uturuki nchini Ujerumani,
bila hata hivyo kutoa ufafanuzi zaidi.
Tayari uhusiano mgumu kati
ya Ujerumani na Uturuki ulishuka zaidi mwezi huu, katika mgogoro
kuhusiana na hatua ya polisi kufuta mikutano ya kisiasa kutafuta
uungwaji mkono katika kura ya maoni ijao. Karibu Waturuki milioni 1.4
wanaoishi Ujerumani wana vigezo vya kupiga kura.
Akitumaini
kutuliza mgororo huo siku ya Jumatano, waziri wa mambo ya nje wa
Ujerumani Sigmar Gabriel alikutana na mwezi wake wa Uturuki Mevlut
Cavusoglu mjini Berlin. Wakati wanadiplomasia hao wawili walikubaliana
juu ya umuhimu wa kudumisha uhusiano mzuri, Cavusoglu alisema Ujerumani
laazima iamuwe sasa iwapo Uturuki ni rafiki au la.
Waziri
wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel (kulia) na mwezi wake wa
Uturuki Mevlut Cavusoglu wakiwa mjini Berlin, 08.03.2017.
Msitari mwekundu
Katika
muktadha wa matamshi kutoka kwa Cavusoglu na rais Erdogan, Gabriel pia
aliweka wazi kwamba katika kuendeleza uhusiano mzuri ipo misitari ambayo
haipaswi kuvukwa. Na mmoja ya misitari hiyo ni kulinganishwa na
Ujerumani ya enzi za manazi, alisema Gabriel.
"Tunataka
kushirikiana vizuri na kwa amani na nchi hii, na kutafuta migogoro
katika njia ya kidemokrasia, kuhakikisha kwamba hakuna mtu anaetendewa
kwa kukosewa heshima, na kwamba wanaweza kutegemea urafiki wa
Wajerumani," alisema Gabriel.
Katika juhudi za kutafuta kuungwa
mkono katika kura ya maoni ya mwezi ujao, Erdogan mwenyewe anatarajiwa
pia kufanya mkutano nchini Ujerumani. Wakosoaji wameonya hata hivyo,
kuwa mfumo unaopendekezwa wa rais ambao unataka kupanua madaraka ya
Erdogan utaimarisha utawala wa mtu mmoja nchini Uturuki.
Ujasusi wa Uturuki nchini Ujerumani
Akisukumwa
na wasiwasi kuhusu mgogoro kati ya Waturuki wa mrengo mkali wa
kizalendo nchini Ujerumani na wafuasi wa chama cha Wakurdi cha PKK, rais
wa BfV Hans-Georg Maassen alianzisha uchunguzi mwezi Januari katika
uwezekano kwamba wahubiri wanaotumwa na Uturuki nchini Ujerumani
wanafanya ujasusi.
Rais wa idara ya upelelezi wa ndani BfV Hans-Georg Maassen.
Maassen
alisema ipo hatari kwamba malumbano hayo ya uwakala kati ya wafuasi wa
PKK na wazalendo wa itikadi kali za mrengo wa kulia, yanaweza kuongezeka
kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa hatari kwa pande zote.
Ingawa
hakuzungumzia moja kwa moja suala la ujasusi wa Uturuki, Maassen
aliwambia waandishi habari mwezi Januari kwamba Ujerumani haitovumia
operesheni ua ujasusi za Uturuki ndani ya mipaka yake. Akirejea matamshi
ya Maassen Jumatano, Gabriel alisema baada ya mkutano wake na
Cavusoglu, kwamba malumbano ya ndani ya Uturuki hayapaswi kuletwa nchini
Ujerumani.
No comments:
Post a Comment