Serikali ya Sudan Kusini ndiyo inayobeba
lawama kubwa kwa baa la njaa linaloshuhudiwa katika baadhi ya sehemu za
nchi hiyo iliyoharibiwa na vita.
Hayo yamesemwa na Umoja wa Mataifa katika kipindi hiki ambapo
mgogoro wa kibinadamu unaoisumbua nchini huyo unakaribia kuwa maafa
makubwa ya kibinadamu.
Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imesema: Serikali ya Sudan
Kusini ndiyo inayobeba lawama kubwa kwa baa la njaa linaloshuhudiwa
katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo huku Rais wa nchi hiyo Salva Kiir
akiendelea kutumia mamilioni ya dola zinazotokana na mauzo ya mafuta
kuimarisha vikosi vyake vya ulinzi.
Umoja wa Mataifa unasema baadhi ya maeneo ya Sudan Kusini
yanakabiliwa na baa la njaa na kwamba karibu nusu ya jamii ya watu wa
nchi hiyo yaani karibu watu milioni tano na laki tano, wanasumbuliwa na
uhaba wa chakula.
Ushahidi unaonesha kuwa, baa hilo la njaa linatokana na machafuko na
vita hususan katika jimbo la Unity, hatua ya jeshi la serikali ya
kuwazuia watoa misaada ya kibinadamu kufika kwenye maeneo yenye njaa na
kukimbia raia kutokana na mapigano ya ndani. Umoja wa Mataifa unasema
kwa uchache nusu ya raia wa Sudan Kusini wamelazimika kuwa wakimbizi
katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka
2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu aliyekuwa makamu
wake, Riek Machar kuwa alifanya jaribio la mapinduzi. Japokuwa
makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka 2015 yalizidisha matumaini
ya kuhitimishwa vita vya ndani lakini machafuko yanayoendelea katika
maeneo mbalimbali ya nchi hiyo yamezusha tena wasiwasi mkubwa na
kusababisha matatizo mengi kwa raia wa kawaida. Makubaliano hayo ya
amani pia yamefutiliwa mbali baada ya kiongozi wa waasi, Riek Machar
kukimbilia nje ya nchi.
Hata hivyo kukimbia kwa Machar hakukuhitimisha vita vya ndani nchini
Sudan Kusini na ripoti mbalimbali zinasema jeshi linalodhibitiwa na Rais
Salva Kiir limekuwa likifanya mauaji ya kikabila. Ripoti ya Umoja wa
Mataifa pia imethibitisha kuwa, mauaji ya kimbari yanafanyika nchini
Sudan Kusini lakini hadi sasa hakujachukuliwa hatua madhubuti za
kukomesha hali hiyo.
Sambamba na hayo Sudan Kusini inasumbuliwa na matatizo makubwa ya
kiuchumi. Mamilioni ya raia wanaishi kama wakimbizi katika maeneo ya
mpakani au kwenye nchi jirani, na wengi miongoni mwao wanasumbuliwa na
uhaba wa chakula na huduma za afya. Mashamba ya kilimo yameharibika na
wakulima wengi wanalazimika kuishi katika kambi za wakimbizi.
Takwimu zinaonesha kuwa, sasa asilimia 42 ya watu wote wa Sudan
Kusini wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na matatizo hayo ya
kiuchumi, vita vya ndani na kusambaratika kwa sekta ya kilimo.
Mgogoro wa Sudan Kusini kwa upande mwingine unachochewa zaidi na
uingiliaji wa madola ya kigeni ambayo yananyonya maliasili na utajiri wa
nchi hiyo changa zaidi barani Afrika. Pato la mafuta la nchi hiyo sasa
linatumika kununua silaha kutoka kwa makampuni makubwa ya nchi za
Magharibi ambazo hapana shaka kuwa hazitaki au kwa uchache hazipendelei
kuona soko la silaha za zana za kivita la Sudan Kusini likitoweka kwa
kupatikana amani na utulivu nchini humo.
Ni kweli kwamba kwa sasa nchi kadhaa za Afrika zinasumbuliwa na baa
la njaa, lakini pia hatuwezi kukanusha kwamba, utendaji mbaya wa
viongozi wa Sudan Kusini umechangia sana katika kuzidisha hali mbaya ya
sasa nchini humo. Baya zaidi ni kuwa, viongozi wa Serikali ya Sudan
Kusini wanawazuia wafanyakazi wa jumuiya ya misaada ya kibinadamu kufika
katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.
Kwa msingi huo inathibitika kuwa, mgogoro wa sasa wa Sudan Kusini ni
matokeo ya siasa mbaya za viongozi wa nchi hiyo zinazosababisha maafa
makubwa kwa raia wa kawaida, na jamii ya kimataifa inalazimika kuchukua
hatua madhubuti zaidi za kukabiliana na viongozi kama hao wasiowajibika.
No comments:
Post a Comment