Wajerumani katika jimbo dogo la Saarland lililoko
magharibi mwa Ujerumani wanapiga kura leo Jumapili katika uchaguzi wa
majimbo ambao unaonekana kuwa kipimo cha umaarufu wa Kansela wa
Ujerumani Angela Merkel.
Uchaguzi wa jimbo la Saarland ndiyo wa kwanza kati ya chaguzi tatu za
majimbo zitakazofanyika kabla ya uchaguzi wa huo wa Septemba 24.
Kwa
maana hiyo unatoa fursa kwa vyama kujenga au kupoteza kasi katika
jitihada zao za kuibuka mshindi katika ngazi ya kitaifa. Kwa sasa jimbo
la Saarland linaongozwa na muungano wa chama cha kihafidhina cha Merkel
CDU na chama cha msimamo wa wastani wa mrengo wa kulia Social Democrat
SPD.
Matokeo ya maoni ya wanachi yaliyotolewa na kituo cha
televisheni cha serikali ZDF yanaonyesha CDU ikiungwa mkono kwa asilimia
37 dhidi ya SPD inayoungwa mkono kwa asilimia 32. Chama cha di Linke
kinachotarajiwa kuungana na SPD kina asilimia 12.5.
Saarland kipimo cha mambo yatakavyokuwa Septemba
Uchaguzi
wa Saarland ndiyo mtihani wa kwanza kwa mgombea Ukansela wa chama cha
SPD Martin Schulz ambaye amekipiga jeki chama hicho tangu kutangazwa
kuwa mgombea wake dhidi ya Merkel. Schulz ameahidi kushughulikia suala
la kukosekana kwa usawa, ambalo wapiga kura wengi wanalichukulia kwa
uzito.
Ramani ya Jimbo la Saarland
Licha
ya kuwa jimbo hilo la Saarland liliko mpakani na Ufaransa lina wakaazi
takriban milioni moja, uchaguzi wake wa leo unachukulika kuwa muhimu
sana katika kupima umaarufu wa Merkel dhidi ya Schulz.
SPD
imejiongezea umaarufu kwa alama 10 kitaifa tangu Schulz kutangazwa
mgombea mwezi Januari akiapa kuufikisha kikomo utawala wa Merkel wa
miaka 12 madarakani. Ushawishi wa Schulz umewavutia hasa wapiga kura
vijana katika nyanja ya kitaifa na katika jimbo la Saarland.
Merkel
aliuambia mkutano wa hadhara alipokuwa akikifanyia chama chake kampeni
katika mji wa Sankt Wendel ulioko mpakani kati ya Ujerumani, Ufaransa na
Luxembourg kuwa kipindi hiki kila kura ina uzito mkubwa.
Kura za
maoni zinabashiri muungano wa SPD, chama cha mrengo wa kushoto cha die
Linke na chama cha wanamazingira wanaoegemea mrengo wa kushoto cha
kijani au muungano wa SPD na Die Linke iwapo chama cha kijani
kitashindwa kupata kura za kutosha katika uchaguzi huo.
Ni CDU au SPD?
Kura
nyingine ya maoni iliyotolewa wiki iliyopita inaonyesha kuwa SPD na
vyama vya kihafidhina CDU na CSU vinaungwa mkono kitaifa kwa asilimia
32. Lakini kura za maoni za Deutschlandtrend zinaonya asilimia 44 ya
wapiga kura wanataka SPD kuongoza serikali ijayo ikilinganishwa na
asilimia 33 ya wanaotaka chama cha Merkel kuongoza.
Mabango yanayoonesha wagombea wa Saarland
Chini
ya utawala wa Merkel Ujerumani imeshuhudia kuimarika kwa uchumi wake na
idadi ya walioajiriwa ikiwa juu lakini pengo kati ya matajiri na
masikini imezidi kuongezeka.
Schulz rais wa zamani wa bunge la
Ulaya mwenye umri wa miaka 61 anajaribu kuwavutia wapiga kura walio
katika tabaka la walioajiriwa, kupitia ujumbe wa matumaini wa kuwepo
usawa na haki za kijamii.
Kura za maoni zinabashiri
kinyang'anyiro kikali kati ya waziri mkuu wa sasa wa Saarland Annegret
Kramp Karrenbauer mwenye umri wa miaka 54, mgombea wa CDU kwa jina la
utani AKK, na naibu wake Anke Rehlinger mwenye umri wa miaka 40 mgombea
wa chama cha SPD.
Vituo vya kupigia kura vinafunguliwa saa mbili
asubuhi na matokeo ya awali yanatarajiwa kutangazwa na vyommbo vikuu vya
habari vya Ujerumani baada ya vituo kufungwa saa kumi na mbili jioni.
No comments:
Post a Comment