Waziri Mshauri katika Masuala ya Ikulu ya
Rais wa Lebanon, amesema kuwa nchi hiyo inaihitajia sana Harakati ya
Hizbullah kwa ajili ya kukabiliana na kuzuia hujuma za utawala haramu wa
Israel na makundi ya kigaidi dhidi ya ardhi ya nchi hiyo.
Sambamba na kusisitizia nafasi chanya ya harakati hiyo ya
muqawama, Pierre Raffoul amesema kuwa, hata katika sherehe za kuapishwa
Rais Michel Aoun alisema kuwa, silaha za Hizbullah si tu kwamba
zinasaidia katika kusimamia usalama ndani ya nchi, bali hata nje ya
mipaka ya Lebanon, zinahusika pia katika kuzuia chokochoko za Israel na
makundi ya kigaidi.
Akifafanua kuwa silaha zinazotumiwa na Hizbullah ni silaha
zinazotumiwa na jeshi la Lebanon, Raffoul amesema kuwa, ni silaha hizo
hizo zilizoweza kuupigisha magoti utawala wa Kizayuni katika vita vya
mwaka 2006. Itakumbukwa katika katika vita vya siku 33, mwaka 2006 kati
ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Lebanon, Israel ilishindwa vibaya
ambapo kutokana na kupata hasara kubwa, ililazimika kurudi nyuma na
kusalimu amri.
Hivi karibuni Rais Michel Aoun akihojiwa na televisheni ya CBC na
gazeti la Misri la al-Ahram alisema kuwa, anaonga mkono kuendelea
ushirikiano wa harakati ya Hizbullah na jeshi la Lebanon, udharura wa
kulindwa silaha za harakati hiyo na uwepo wa Hizbullah nchini Syria
katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi na ukufurishaji ili kulinda
taifa la Lebanon.
Aidha hivi karibuni Alexander Zasypkin, balozi wa Russia nchini
Lebanon alisema kuwa, tangu awali harakati ya Hizbullah imekuwa na
nafasi muhimu na chanya katika kupambana na magaidi nchini Syria na
kudumisha usalama nchini Lebanon.
No comments:
Post a Comment