Amri mpya iliyotolewa na Rais Donald Trump wa
Marekani ya kupiga marufuku raia wa nchi sita za Waislamu kuingia
nchini humo imeendelea kupingwa kisheria na majimbo ya nchi hiyo baada
ya Mwanasheria Mkuu wa jimbo la Washington kuungana na jimbo la Hawaii
kuchukua hatua ya kuzuia utekelezaji wake.
Mwanasheria
Mkuu wa jimbo la Washington Bob Ferguson, ambaye alikuwa mtu wa mwanzo
kukwamisha amri ya marufuku ya kwanza iliyotangazwa na Trump amesema,
amri mpya ya sasa pia inakiuka Katiba ya Marekani kwa kuwa "haiutendei
ipasavyo Uislamu".
Amesema
hoja iliyowasilishwa na ofisi yake inataka zuio dhidi ya amri ya mwanzo
iliyotangazwa na rais wa Marekani mnamo mwezi Januari litekelezwe pia
kuhusiana na dikrii yake mpya.
Hii
ni katika hali ambayo Wanasheria Wakuu wa majimbo ya New York,
Massachusetts na Oregon wametangaza kuwa nao pia wameshachukua hatua ya
kujiunga na shauri la kisheria lililowasilishwa mahakamani na jimbo la
Washington pamoja na Minnesota kupinga marufuku iliyotangazwa na Trump.
Amri hiyo mpya iliyotangazwa siku ya Jumatatu baada ya kufanyiwa
marekebisho na ambayo inatarajiwa kuanza kutekelezwa tarehe 16 mwezi huu
inapiga marufuku kutoa viza za kuingia Marekani watu wanaotoka Syria,
Iran, Somalia, Libya, Sudan na Yemen na kufunga kwa muda wa siku 120
mpango wa Marekani kwa ajili ya wakimbizi.
Mwanasheria
Mkuu wa Oregon Ellen Rosenblum amesema amri hiyo ya Rais wa Marekani
imeathiri jimbo hilo, wakaazi wake, waajiri, taasisi za elimu, mfumo wa
huduma za afya pamoja na uchumi.
Mwanasheria Mkuu wa jimbo la New York Eric Schneiderman amesema, kwa jina jingine amri hiyo ni "marufuku dhidi ya Waislamu"
Shauri
la kisheria lililowasilishwa na jimbo la Hawaii limeeleza kuwa amri ya
Trump itaathiri jamii ya Waislamu wa jimbo hilo, utalii pamoja na
wanafunzi wa kigeni…/
No comments:
Post a Comment