Shirika la kimataifa la Haki za Binadamu HRW limetaka Rais Omar al Bashir wa Sudan azuiwe kuingia nchini Jordan.
Kwa mujibu wa shirika la habari la
AFP, Human Rights Watch imetoa tamko la kuitaka serikali ya Jordan imma
imzuie Rais Omar al Bashir kutembele nchi hiyo au imtie mbaroni mara
atakapowasili nchini humo.
Taasisi hiyo ya kimataifa isiyo ya
kiserikali imegusia tuhuma zinazomkabili Rais wa Sudan za kuhusika
katika jinai za kivita za jimbo la Darfur la magharibi mwa nchi hiyo na
kuitaka serikali ya Jordan iheshimu makubaliano ya kimataifa.
Katika tamko lake hilo Human Rights Watch imesema, kwa vile Jordan ni
mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, ina wajibu wa
kutekeleza makubaliano yaliyounda mahakama hiyo. Shirika hilo la haki za
binadamu limedai pia kuwa, kama Jordan itamruhusu Rais al Bashir
kutembelea nchi hiyo au kama haitomtia mbaroni, itakuwa imekwenda
kinyume na ahadi zake kwa mujibu wa makubaliano ya ICC.
Mahakama ya ICC inadai kuwa Rais Omar al
Bashir wa Sudan amehusika katika jinai za kivita katika jimbo la Darfur
na imetoa waranti wa kutiwa mbaroni.
Kikao cha wakuu wa Jumuia ya Nchi za
Kiarabu kimepangwa kufanyika Jumatano ya tarehe 29 mwezi huu wa Machi
nchini Jordan. Rais Omar al Bashir amealikwa kushiriki kwenye kikao
hicho.
Jimbo la Darfur la magharibi mwa Sudan
lilikumbwa na machafuko tangu mwaka 2003 kulalamikia kudharauliwa na
kutelekezwa na serikali.
No comments:
Post a Comment