Kauli mbiu ya mwaka huu wa 2017 inasema "Misitu na
Nishati" ikiwa ni mahsusi kutokana na uwekezaji mkubwa katika uvumbuzi
wa teknolojia na usimamizi endelevu wa misitu kama suala muhimu.
Katika kuiadhimisha siku ya kimataifa ya misitu kila mwaka, nchi
mbalimbali duniani zinahamasishwa kuendeleza juhudi za kitaifa na
kimataifa ili kuandaa na kushiriki katika shughuli zinazohusika na
misitu pamoja na miti, kama vile kampeni ya kupanda miti pamoja na
midahalo kuhusu misitu. Siku hii huadhimishwa kwa ajili ya kuwafanya
watu waelewe umuhimu wa aina zote za misitu duniani, ikiwemo jukumu lake
katika mabadiliko ya tabia nchi.
Uwekezaji na usimamiizi endelevu wa misitu
Kwa
mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO,
kaulimbiu ya mwaka huu ya 'Misitu na Nishati', imechaguliwa kutokana na
uwekezaji mkubwa katika uvumbuzi wa teknolojia na katika usimamizi
endelevu wa misitu kuwa suala muhimu katika kuongeza nafasi ya misitu
kama chanzo kikuu cha nishati mbadala.
Mwanaharakati wa mazingira kutoka nchini Kenya ambaye sasa ni marehemu Wangari Maathai
Kulingana
na suala hilo, uwekezaji sasa unaangaziwa zaidi katika mustakabali
endelevu ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu na kukuza uchumi wa
kijani. Kwa mujibu wa FAO, kuongezeka kwa kaya na jamii yenye vitalu vya
miti pamoja na matumizi ya majiko ya kutumia kuni, kunaweza kuwapatia
mamilioni ya watu zaidi katika nchi zinazoendelea urahisi wa kupatikana
kwa nishati mbadala ambayo ni nafuu na yenye kuaminika.
Maadhimisho ya mwaka huu
Shirika
la FAO litaiadhimisha siku hii katika makao makuu ya shirika hilo mjini
Roma, Italia, ambapo mkurugenzi wake mkuu, Jose Graziano da Silva,
atafungua maadhimisho hayo. Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa katika
maadhimisho haya ni pamoja na majukumu ya misitu na nishati ya kijani
katika utekelezaji wa makubaliano ya Paris ya Nationally Determined
Contributions, NDCs, ambayo itatolewa na Rais wa Jamhuri ya Fiji, Jioji
Konusi Konrote.
Ukutaji wa miti kwa ajili ya matumizi mbalimbali ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa misitu
Aidha,
Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Kuenea kwa
Jangwa, UNCCD, Monique Barbut, atatoa mada kuhusu suala la kufungamana
kwa misitu na nishati, ambalo ni suala muhimu la maendeleo endelevu
pamoja na ushujaa katika maisha ya watu. Eva Müller, Mkurugenzi wa Idara
ya Sera za Misitu na Ugavi wa Rasilimali katika shirika la FAO,
atazindua chapisho la FAO ambalo linazungumzia kipindi cha mpito cha
matumizi ya mkaa: thamani ya mkaa katika kukabiliana na mabadiliko ya
tabia nchi na kuimarisha maisha ya watu.
Aidha, Müller atatoa
mada kuhusu ajenda inayochukuliwa na FAO katika misitu na nishati ya
kijani. Naye Makamu wa Rais wa shirika la Metsa, Rikka Joukio, atatoa
mada kuhusu mustakabali wa nishati katika jamii katika kuuvumbua mtazamo
huo. Maadhimisho hayo yatahitimishwa kwa hotuba itakayotolewa na Maria
Helena Semedo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Hali ya Hewa na Maliasili wa
FAO.
Siku hii ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2012 na siku hiyo ilisherehekewa kwa mara ya kwanza Machi 21, 2013.
No comments:
Post a Comment