Sunday, March 26, 2017

MAANDAMANO SANA'A KULAANI VITA VYA SAUDIA DHIDI YA YEMEN

Mamilioni ya wananchi wa Yemen wameandamana leo katika mji mkuu Sana'a na maeneo mengine nchini humo katika mwanzo wa mwaka wa tatu tokea Saudia ianzishe vita vyake vya kinyama dhidi ya nchi hiyo ambavyo vimesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wengine wengi kupoteza makazi yao.
Katika maandamano hayo yaliyofanyika leo Jumapili katika Medani ya Al Sabin mjini Sana'a, Wayemen walikuwa wamebeba bendera za nchi yao huku wakitoa nara dhidi ya umwagaji damu unaofanywa na Saudia nchini humo kwa muda wa miaka miwili.
Akizungumza katika maandamano hayo, Saleh al Samad, Rais wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amewapongeza Wayemen kwa kusimama kidete kupambana na wavamizi wa Aal Saud. Amesema Saudi Arabia imeshindwa kufikia malengo yake nchini Yemen pamoja na kuwa imetumia kiasi kikubwa cha fedha na silaha za kisasa.
Lengo kuu la mashambuliai ya Saudia dhidi ya Yemen ni kumrejesha madarakani kibaraka wake, Rais wa zamani wa nchi hiyio aliyejiuzulu na kutoroka nchi Abdu Rabuh Mansour Hadi. Lengo jingine ni kutaka kuwaondoa madarakani wanamapinduzi wa Ansarullah.
Uharibifu wa Saudia katika makazi ya raia nchini Yemen
Tangu ulipoanzisha uvamizi wake wa kijeshi dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka 2015 hadi sasa, muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na utawala wa Aal Saud na kuungwa mkono na Marekani na Israel umeshaua zaidi ya watu 12,000 katika mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu. Kwa mujibu wa televisheni ya Al Masira, kati ya waliopoteza maisha katika hujuma ya Saudia ni watoto 2,646 na wanawake 1,922.
Aidha  muungano huo vamizi umeshazishambulia skuli, hospitali, makaazi ya raia, barabara, masoko na kambi za wakimbizi na kuua maelfu ya raia wasio na hatia wa Yemen. Ndege za kivita za Saudia aidha zimebomoa nyumba za raia zipatazo 403,039 na misikiti 712.

No comments:

Post a Comment