Umoja wa Ulaya (EU) umetaka Umoja wa Mataifa
uanzishe uchunguzi kuhusu mateso, ubakaji na mauaji yaliyofanywa dhidi
ya jamii ya wachache ya Waislamu Warohingya nchini Myanmar.
Rasimu ya azimio ambayo Umoja wa Ulaya umeiwasilisha kwenye
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa hapo jana la kuanzishwa
uchunguzi wa kimataifa nchini Myanmar imetumia lugha kali zaidi kuliko
rasimu inayofanana na hiyo iliyowasilishwa na EU hapo kabla.
Ripoti ya mwezi uliopita ya Umoja wa Mataifa iliyoandaliwa kulingana
na ushahidi uliotolewa na manusura waliokuweko nchini Bangladesh
inaonyesha kuwa jeshi na polisi ya Myanmar wametenda jinai dhidi ya
Waislamu wa jamii ya wachache ya Rohingya kwa namna ya kuangamiza kizazi
na jinai dhidi ya binadamu.
Aidha itakumbukwa kuwa ripoti iliyotolewa na shirika la kutetea haki
za binadamu la Human Rights Watch imeeleza kuwa kwa akali nusu ya
wanawake na mabinti 101 wa Kiislamu wa jamii ya Rohingya waliohojiwa na
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa walisema
kuwa, walibakwa na kunajisiwa na askari wa serikali ya Myanmar.
Tarehe 23 na 24 za mwezi huu wa Machi, Baraza la Haki za Binadamu la
Umoja wa Mataifa linatazamiwa kuipigia kura rasimu ya azimio
lililorejeshwa tena mbele ya baraza hilo kuhusu hali ya Waislamu wa
Rohingya nchini Myanmar.
Umoja wa Mataifa umewataja Waislamu wa Myanmar kuwa jamii ya wachache inayokandamizwa zaidi dunaini..
No comments:
Post a Comment