Marekani imetoa tishio la vita vya kibiashara
dhidi ya dunia. Waziri wa Biashara wa Marekani Wilbur Ross amesema
Marekani imekuwa katika vita vya kibiashara kwa miongo kadhaa lakini
sasa nchi hiyo iko tayari kutumia uwezo wake wote kujibu mapigo.
Hivi sasa uchumi wa Marekani unakabiliwa na nakisi ya bajeti
ya takribani dola bilioni 800 huku mlingano wa kibiashara ukiwa ni kwa
faida ya madola ya kigeni. Mwaka 2014, kwa kila dola trilioni moja na
bilioni 500 ambazo ni thamani ya mauzo ya nje ya Marekani, nchi hiyo
imekuwa ikinunua huduma na bidhaa kutoka nje zenye thamani ya trilioni
mbili na dola bilioni 300.
Katika mlingano wa mabadilishano ya kibiashara, China inaiongoza
Marekani kwa dola bilioni 340, Umoja wa Ulaya bilioni 142, Japan bilioni
167, Mexico bilioni 53 na Canada bilioni 35. Kwa msingi huo nchi hizo
zinauiuzia Marekani bidhaa na huduma zaidi ya Marekani inavyoweza
kuziuzia.
Kiu isiyokwisha ya Wamarekani ya kutaka kutumia kwa wingi bidhaa
kiholela ni jambo ambalo limepelekea nchi hiyo kukumbwa na wimbi la
mmiminiko wa bidhaa za kigeni. Halikadhalika gharama za uzalishaji
bidhaa Marekani ziko juu sana ikilinganishwa na maeneo mengine ya dunia;
na ni kwa sababu hii ndio maana Wamarekani wanafadhilisha kununua
bidhaa za kigeni ambazo zinauzwa kwa bei nafuu.
Sheria ngumu za kuajiri wafanyakazi pamoja na mfumo mbaya wa ushuru
ni mambo ambayo yamepelekea wazalishaji bidhaa Marekani kutoweza
kushindana na wenzao wa kigeni.
Takwimu zinaonyesha kuwa, Marekani ndio nchi yenye uchumi mkubwa
duniani na moja ya nchi muhimu zaidi kiviwanda. Pamoja na hayo miongoni
mwa sekta 11 muhimu za kiviwanda, Marekani imeweza kufanikiwa katika
sekta tatu tu ambazo ni sekta ya dawa, sekta ya plastiki na sekta ya
utengenezaji ndege. Katika upande wa pili Marekani inaagiza kutoka nchi
zingine duniani bidhaa muhimu kama vile bidhaa za elektroniki, mashine
za viwanda, magari na petroli na hivyo kupelekea uchumi wa nchi hiyo
kudhoofika.
Hivi sasa kwa kuzingatia matatizo katika muundo wa kiuchumi wa
Marekani na uraibu wa kutumia bidhaa kupindukia (consumerism) walionao
raia wa nchi hiyo, wakuu wa Washington sasa wanataka kuanzisha vita vya
kibiashara na mataifa mengine duniani.
Katika miaka ya nyuma, Marekani pia ilikuwa na ushindani mkubwa na
baadhi ya washirika wake wa kibiashara hasa Japan na China. Hivi sasa
serikali ya Marekani imeweka kando udiplomasia na imetangaza wazi vita
vya kibiashara. Hivi sasa mbali na matokeo tarajiwa ya vita vya
kibiashara baina ya madola makubwa duniani, nukta nyingine muhimu ni
kuwa, Marekani haiwezi kuibuka mshindi hadi pale itakapo badilisha
muundo wake wa kiuchumi na kuweza kudhibiti utamaduni mbovu wa watu wake
kutumia bidhaa kiholela na kupita kiasi.
Tab'an Rais Donald Trump amechukua hatua kuekelea katika marekebisho
hayo kwa kutoa nara kama vile 'Marekani Ipewe Kipaumbele', 'Nunua Bidhaa
za Marekani' , 'Ajiri Mmarekani' n.k. Lakini kuna shaka kubwa iwapo
wazalishaji bidhaa, wafanya biashara wakubwa na raia wa Marekani
wataafiki kutekeleza mabadiliko hayo. Ni kwa sababu hii ndio maana
badala ya serikali ya Marekani kujikita katika kuleta mabadiliko ndani
ya nchi imechukua mkondo wa kuibua utata katika uchumi na biashara ya
kimataifa kwa kutumia mabavu ili kujaribu kuzuia kuporomoka
kusikoepukika kwa nchi hiyo katika uga wa kimataifa.
No comments:
Post a Comment