Jumatatu ya tarehe 27 Novemba, Papa Francis,
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani aliwasili Yangon mji mkubwa kabisa
wa Myanmar akianza safari ya siku nne ya kuitembelea nchi hiyo mashariki
mwa Asia.
Safari ya Papa nchini Myanmar
inafanyika baada ya kupita miezi mitatu tangu kuanza duru mpya ya
uangamizaji kizazi cha jamii ya waliowachache ya Waislamu Warohingya.
Mamia ya Wakatoliki walijitokeza kumlaki kiongozi huyo wa Kanisa
Katoliki Duniani wakati alipowasili katika mji huo. Nchini Myanmar kuna
Wakatoliki takribani laki saba katika jamii ya watu milioni 51 wa nchi
hiyo. Wakristo hao Wakatoliki wanaishi kwa amani kamili nchini humo.
Lakini Waislamu milioni moja wa jamii ya
Rohingya ambao wanapatikana katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa
Myanmar wamekuwa wakikabiliwa na ubaguzi na ukatili mkubwa pamoja na
hujuma za mabudha wanaopata uungaji mkono wa serikalim katika ukatili
wao dhidi ya Waislamu. Mabudha wakipata uungaji mkono wa moja kwa moja
wa jeshi la Myanmar wameanzisha duru mpya ya mauaji, mateso, ubakaji wa
mabinti na wanawake na kupelekea mamia ya maefu ya Waislamu hao kuwa
wakimbizi.
Serikali ya Myanmar, haiwatambui Waislamu wa jamii ya Rohingya kwamba
ni raia wa nchi hiyo bali inawaona kuwa ni wahajiri kutoka nchi jirani
ya Bangladesh. Kabla ya kufanya safari hiyo, Askofu wa Myanmar alimtaka
Papa Francis kutotumia neno Rohingya atakapokuwa safarini nchini humo,
ili kuzuia kuibua hasira za viongozi wa serikali. Duru mpya ya
uangamizaji kizazi cha Waislamu wa jamii ya Rohingya ilianza katika hali
ambayo, jinai kama hizo hazijawahi kushuhudiwa nchini Mynamar tangu
nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1948 ambapo kabla ilikuwa ikijulikana kwa
jina la Burma.
Katika kipindi cha miaka 70 iliyopita ya utawala wa Mabudha nchini
humo, daima umekuwa ukitaka kukifuta kikamilifu kizazi cha jamii ya
Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine. Katika kipindi hicho
Waislamu hao wameshambuliwa zaidi ya mara 20 kwa aina mbalimbali ya
mashambulio. Sambamba na mashambulio hayo, kumekuweko na njama mtawalia
za kuwanyima Waislamu hao haki za kiraia lengo likiwa ni kuwafuta katika
ramani ya nchi hiyo.
Umoja wa Mataifa umetangaza katika ripoti yake kwamba, Waislamu wa
Rohinga ndio jamii ya wachache ulimwenguni iliyodhulumiwa zaidi. Tangu
kuanza kwa duru mpya ya mauaji ya kizazi na utokomezaji kizazi cha jamii
ya Waislamu wa Rohingya, zaidi ya Waislamu elfu moja wameuawa kikatili,
makumi ya maelfu ya wanawake wamebakwa na kunajisiwa huku wengine
takribani laki sita na ishirini elfu wakilazimika kuyahama makazi yao na
kukimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh. Waislamu Warohingya
waliokimbilia Bangladesh nao wanakabiliwa na hali mbaya katika kambi za
muda walizopatiwa kutokana na kukosa huduma muhimu za kuendeshea maisha.
Licha ya Umoja wa Mataifa na asasi za
kutetea haki za binadamu kukiri bayana katika ripoti zao nyingi juu ya
kutokea maafa ya kibinadamu nchini Myanmar na hali mbaya inayowakabili
wakimbizi wa Kirohingya huko Bangladesh, lakini serikali ya Myanmar na
hata shakhsia wake mashuhuri Aung San Suu Kyi ambaye ana Tuzo ya Amani
ya Nobel wanakana kabisa juu ya kuweko muamala mbaya dhidi ya Waislamu
wa nchi hiyo.
Matamshi ya madola ya Magharibi, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani
na viongozi wa Myanmar hususan Aung San Suu Kyi kuhusiana na
kuhitimishwa siasa za uangamizaji kizazi dhidi ya Waislamu wa Rohingya
na kuandaliwa mazingira ya kurejea wakimbizi wa jamii hiyo kutoka
Bangladesh ni matarajio na utafadhalishaji. Viongozi hao badala ya
kuzingatia ripoti mbalimbali za Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wake
kuhusiana na hali mbaya ya Waislamu Warohingya, wamekuwa wakiyapa
kipaumbele matamshi ya serikali ya Myanmar.
Hivi kama badala ya Waislamu wa
Rohingya, Wakristo wa nchi hiyo ndio ambao wangekuwa wanakabiliwa na
siasa hizo za uangamizaji kizazi, Papa na viongozi wa madola ya
Magharibi wangekuwa wanatoa matamshi kama wanayotoa hivi sasa? Je Aung
San Suu Kyi angeendelea kuonekana kuwa ni fakhari kutokana na kupata
Tuzo ya Amani ya Nobel? Waislamu wa jamii ya Rohingya wanauawa na
wengine kulazimika kuwa wakimbizi na madola ya Magharibi yamenyamzia
kimya hilo kutokana na kuwa wanaofanyiwa jinai hizo ni Waislamu na si
vinginevyo.
No comments:
Post a Comment