Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu katika masuala ya kimataifa amemuonya Rais Emmanuel Macron wa
Ufaransa asiingilie masuala ya ndani ya Iran kwani kujiingiza katika
masuala yasiyomuhusu hakuna faida kwa nchi yake.
Ali Akbar Velayati amesema hayo
leo wakati alipohojiwa na shirika la habari la IRIB na sambamba na
kumlaumu Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwa kuingilia masuala ya
ulinzi ya Iran amesema, kitendo cha Paris cha kujiingiza katika suala la
makombora ambalo ni la kiistratijia kwa Iran hakina matunda yoyote
isipokuwa kuzidi kujipotezea heshima Ufaransa mbele ya Jamhuri ya
Kiislamu.
Mshauri huyo wa Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amesisitiza kuwa, Iran
haiombi idhini ya mtu yeyote katika masuala yake ya kiulinzi na kusema
wazi kwamba, kama Ufaransa inataka kuwa na uhusiano mzuri na Iran basi
inapaswa iache kujiingiza katika masuala yake ya ndani kwani ni kinyume
na maslahi ya kitaifa ya Ufaransa.
Amesisitiza kuwa, bila ya shaka yoyote
majibu ya Iran kuhusu mwito wa Ufaransa juu ya mradi wake wa makombora
ni hapana na hakuna hata uwezekano wa asilimia moja wa kukubaliana na
jambo hilo.
Jana Ijumaa, Rais wa Ufaransa alidai eti
kuna haja kwa Iran kuweka wazi stratijia zake za mradi wa makombora ya
balestiki na kudai kuwa Iran inapaswa kuachana na siasa zake alizoziita
eti ni za mashambulizi.
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amemjibu rais
huyo wa Ufaransa na kumuonya asiingilie masuala ya ndani ya Iran kwani
kila nchi ina haki ya kujilinda na kwamba nchi yoyote ile haina haki ya
kuipangia itumie stratijia gani katika kuimarisha nguvu zake za ulinzi.
No comments:
Post a Comment