Makamu wa Rais wa Marekani ameyataja maghala ya silaha za nyuklia za nchi hiyo kuwa suala linalopelekea kuwepo amani duniani.
Akiwa ziarani kukitembelea kituo
cha jeshi la anga cha Minot, Mike Pence Makamu wa Rais wa Marekani
amesema hakuna nguvu duniani inayopelekea kuwepo amani sawa na maghala
ya silaha za nyuklia za Marekani.
Matamshi hayo yametolewa katika hali
ambayo Marekani inatambulika ulimwenguni kama nchi pekee inayotumia
silaha za nyuklia vitani. Miaka 70 iliyopita Wamarekani waliishambulia
kwa mabomu ya nyuklia miji miwili ya Hiroshima na Nagasaki huko Japan na
kusababisha vifo vya raia wa nchi hiyo zaidi ya laki tatu baada ya
kupitia mateso na masaibu chungu nzima. Kabla ya wakati huo, hakukuwa na
silaha yoyote ya kivita iliyotengenezwa na binadamu iliyosababisha
mauaji ya kutisha kama hayo. Mashambulizi hayo ya nyuklia yalizua hofu
kubwa duniani kwa kadiri kwamba kwa mara ya kwanza katika historia,
mwanadamu alikumbwa na wasiwasi wa kuangamizwa dunia nzima.
Miaka minne tu baada ya Marekani kufanya
mashambulio hayo ya nyuklia huko Japan, Umoja wa Kisovieti ulilifanyia
jaribio bomu lake la kwanza la nyuklia na ni baada ya hapo ndipo
kukaanza zama za ushindani wa silaha za nyuklia duniani. Ushindani huo
mkubwa uliendelea na kuzifanya nchi mbili za Marekani na Urusi ya zamani
mwezi Oktoba mwaka 1962 kukaribia kupigana vita vya nyuklia. Wakati huo
kama Urusi ya zamani isingezirejesha karibu na Cuba meli zake
zilizokuwa zimebeba makombora ya nyuklia, labda Rais wa wakati huo wa
Marekani John F. Kennedy angeamuru kupiganwa vita vya nyuklia; vita
ambavyo katika masaa yake ya awali vingeweza kuua kwa uchache watu
milioni 400. Marekani pekee hivi sasa imerundika katika maghala yake ya
silaha, silaha za nyuklia ambazo zina uwezo wa kuiharibu dunia mara
kadhaa. Hata kama Marekani katika miaka 70 iliyopita haijatumia silaha
za aina hiyo, lakini imehusika kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya
moja kwa moja katika kuenea kwa silaha hizo hatari. Dunia sasa inahofia
makabiliano ya kinyuklia kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini ambayo
yanaweza kusababisha maafa makubwa kati ya pande mbili.
Hasa ikitiliwa maanani kuwa amani ya
dunia anayoikusudia Pence haitokani na uadilifu na ridhaa ya jamii, bali
inatokana hofu ya Marekani kutekeleza mashambulizi ya nyuklia dhidi ya
nchi nyingine. Kuwepo hofu na wasiwasi wa kusambaratika kikamilifu
madola makubwa duniani miaka 70 baada ya kumalizika Vita vya Pili vya
Dunia kumezuia kuibuka migogoro kati ya madola hayo. Wakati huohuo nchi
zilizokuwa zikimiliki nguvu za nyuklia kama Marekani zilihamisha uhasama
na mashindano yao ya kijeshi kutoka ndani ya ardhi za nchi hizo na
kuyahamishia katika maeneo yaliyobaki nyuma kimaendeleo na yale
yaliyokuwa yakistawi huko Asia, Afrika na Amerika ya Latini. Watu wa
maeneo hayo walipoteza maisha na kugharimika pakubwa kufuatia vita hivyo
baina ya madola makuu duniani. Kwa ibara nyingine ni kuwa, amani
iliyoipata Marekani kwa silaha zake za nyuklia na waitifaki wake wa
Ulaya haijakuwa na natija nyingine ghairi ya kusababisha vita na
umwagaji damu katika maeneo mengine ya dunia
No comments:
Post a Comment