Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka
ya Kenya IEBC Wafula Chebukati amemtangaza Uhuru Kenyatta, mgombea
urais kwa tiketi ya chama cha Jubilee Rais mteule na mgombea wake mwenza
William Ruto kuwa Naibu Rais mteule baada ya kupata ushindi wa kishindo
katika uchaguzi wa marudio wa rais uliofanyika siku ya Alkhamisi.
Akitangaza matokeo hayo jioni ya leo, Chebukati alisema uchaguzi huo ulikuwa huru, halali na wa haki.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti huyo wa IEBC,
Kenyatta amejinyakulia kura 7,483,895 ambazo ni sawa na asilimia 98.27
ya kura zote halali zilizopigwa katika uchaguzi huo wa rais ambao
ulisusiwa na mpinzani wake mkuu Raila Odinga.
Zoezi la kutangaza matokeo limefanyika bila kujumuisha majimbo 25 ya
mkoa wa Nyanza ambayo yalishindwa kupiga kura siku ya Alkhamisi kutokana
na fujo na machafuko yaliyokwamisha upigaji kura katika majimbo hayo.
Chebukati amesisitiza kuwa masharti yaliyokuwa yamewekwa na Mahakama
ya Juu iliyofuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa Agosti 8 kwa ajili ya
uchaguzi wa marudio yametekelezwa, hivyo uchaguzi huo ni halali, huru na
wa haki.
Aidha amesema uchaguzi wa marudio wa rais umeendeshwa na timu mpya
iliyojumuisha wafanyakazi wa IEBC kutoka kila pembe ya nchi. Ameongeza
kuwa hali katika majimbo 25 ya mkoa wa Nyanza ilisababisha uchaguzi
ushindwe kufanyika katika maeneo hayo.
Akizungumza mapema leo, Naibu Mwenyekiti wa IEBC Consolata Nkatha
alisema kura za maeneo ambayo uchaguzi haukufanyika hazitoathiri matokeo
rasmi ya uchaguzi huo.
Mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa upinzani wa NASA Raila Odinga
alisusia uchaguzi wa marudio akitaka pamoja na mambo mengine kutimuliwa
maafisa waandamizi wa tume ya uchaguzi na kubadilishwa wachapishaji wa
karatasi za kupigia kura na watayarishaji wa teknolojia itakayotumika
katika mchakato wa uchaguzi huo.
Hayo yanajiri huku Wakenya wakisubiri kwa hisia tofauti msimamo wa
kiongozi huyo wa upinzani ambao ameahidi kuutangaza baada ya rais
Kenyatta kutangazwa rasmi mshindi wa uchaguzi wa marudio.../
No comments:
Post a Comment