Mabadiliko yanayojiri kwenye medani za vita
nchini Iraq yanabainisha kusambaratishwa na kutokomezwa Daesh (ISIS)
nchini humo; na kushindwa kikamilifu kundi hilo la kigaidi na kitakfiri
ambako ni sawa na kupata mafanikio makubwa Wairaqi katika mapambano
dhidi ya magaidi kumeakisiwa sana na duru mbalimbali za habari.
Vikosi vya jeshi la Iraq siku ya Ijumaa viliukomboa mji wa
Rawah kutoka kwenye makucha ya magaidi wa Daesh. Kufuatia kukombolewa
mji huo kulikochukua muda wa saa kadhaa tu, Waziri wa Mambo ya Ndani wa
Iraq Qasim Al-Araji alitangaza kuwa kundi la kigaidi na ukufurishaji la
Daesh limesha sambaratishwa kikamilifu nchini humo. Rawah ilikuwa
miongoni mwa ngome za mwisho za Daesh ndani ya ardhi ya Iraq. Hivi sasa
magaidi wa kundi hilo la ukufurishaji hawana mji mwengine wowote muhimu
wa Iraq wanaoushikilia na kuukalia kwa mabavu isipokuwa wanaishia
kuzunguka zunguka na kuranda randa kwenye maeneo ya mbali na
katika baadhi ya vijiji.
Mnamo mwaka 2014, kwa uungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Marekani
na waitifaki wake wa Magharibi na wa Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia,
kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh liliishambulia Iraq, likayavamia
na kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya kaskazini na magharibi mwa
nchi hiyo. Lakini tangu wakati huo hadi sasa, jeshi la Iraq lilkisaidiwa
na vikosi vya kujitolea vya wananchi limeweza kuyakomboa maeneo hayo
kutoka kwenye makucha ya kundi hilo; na kimsingi kundi hilo
limeshasambaratishwa kikamilifu nchini humo.
Hata hivyo baada ya kushindwa kijeshi kundi la kigaidi na
ukufurishaji la Daesh, suali la kujiuliza hivi sasa ni je, kwa ushindi
huo, Wairaqi sasa wataweza kupumua na kupata salama ya kuepukana na
shari ya ugaidi? Au kundi hilo la kigaidi na kitakfiri litaanzisha mbinu
nyengine mpya na kuendelea kuwaandamana wananchi wa Iraq kwa hujuma na
jinai zake za kinyama? Kwa kuzingatia kuwa mashambulio ya kigaidi
yalishadidi hivi karibuni katika nchi za Iraq na Syria, tunaweza kusema
kuwa baada ya kushindwa kijeshi na kupoteza maeneo waliyokuwa
wakiyashikilia kwa mabavu, magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh
wameshaainisha mkakati wanaokusudia kuutekeleza mnamo siku zijazo. Ili
kufifisha kushindwa kwake kijeshi, kundi la Daesh (ISIS) limeanzisha
mbinu na mkakati wa kuvuruga usalama, kwa kushadidisha mashambulio ya
kujitoa mhanga ya miripuko ya mabomu pamoja na mauaji ili kuvuruga amani
na uthabiti nchini Iraq, sambamba na kupanua wigo wa harakati zake
katika nchi nyengine ikiwemo Afghanistan, Libya na kwengineko. Harakati
za aina hiyo ni muendelezo wa njia na misimamo ya kufurutu mpaka
iliyoanzishwa mwaka 2004 na Abu Mus'ab Az-Zarqawi kwa njia ya kuanzisha
mauaji na kuwalenga raia; na baada ya kushadidi hitilafu baina ya
Wairaqi ikaandaa mazingira ya kuzaliwa Daesh kutoka kwenye tumbo la
Al-Qaeda na kupelekea hatimaye mwaka 2014 kushambuliwa na kukaliwa kwa
mabavu kirahisi miji mbalimbali ya ardhi ya Iraq.
Leo hii baada ya miaka mitatu ya vita na mapigano makali ya kujitolea
mhanga, yaliyowagharimu roho nyingi za watu na kuwasababishia pia
uharibifu mkubwa, Wairaqi wameweza kuyakomboa maeneo yote ya ardhi yao
yaliyokuwa yamevamiwa na kushikiliwa kwa mabavu na Daesh; hata hivyo
ushindi huo wa kijeshi dhidi ya magaidi wenye misimamo ya kufurutu mpaka
sio mwisho wa mapambano, bali inapasa ifanyike kazi ya kuing'oa na
kuitokomeza mizizi ya misimamo hiyo hatari. Katika hali kama hiyo,
inavyoonekana, baada ya kulisambaratisha kijeshi kikamilifu kundi la
Daesh nchini Iraq, vita na mapambano yajayo yatakuwa ni ya kitaarifa na
kiintelijinsia ambayo hayatotegemea askari na vifaru pekee; bali
yatategemea zaidi unasaji wa taarifa za kiintelijinsia. Katika mazingira
ya sasa ambapo magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh wamesha
sambaratishwa kikamilifu nchini Iraq, Marekani, ambayo inahisi njama na
mipango yake iliyokuwa imepanga dhidi ya Iraq na eneo kwa jumla
imevurugika, hivi sasa inashughulika kupanga njama na mikakati mingine
mipya ya kiadui.
Ukweli ni kwamba kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh
limeshafutwa kwenye ramani ya Iraq, na hilo limewezekana kwa baraka na
nafasi ya uongozi wa juu wa kidini na kwa kujitolea mhanga vikosi vya
Iraq hususan vya jeshi la kujitolea la wananchi la Al Hashdu-Sha'abi. Na
hii ni katika hali ambayo jeshi hilo la wananchi lingali linaendelea
kuandamwa na njama na tuhuma za Marekani. Kutokana na matukio yaliyojiri
huko Iraq wananchi wanapaswa kuwa macho zaidi katika kipindi
kinachoanza hivi sasa cha baada ya kusambaratishwa Daesh nchini humo.../
No comments:
Post a Comment