Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye yuko
katika ncha ya kuuzuliwa amekataa kuachia madaraka akisisitiza kuwa yeye
ndiye kiongozi halali wa nchi hiyo.
Duru za habari zimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa,
Mugabe amekataa upatanishi wa Askofu wa Kanisa Katoliki nchini
humo Fidelis Mukonori, ambaye alikuwa anaongoza mazungumzo kati ya rais
huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 93 na makamanda wa jeshi la nchi hiyo.
Jeshi hilo jana lilitangaza kuwa Mugabe na familia yake wako kwenye
kizuizi cha nyumbani na kuongeza kuwa litawapandisha kizimbani wale
liliowataja kama "wahalifu" waliomzunguka kiongozi huyo ambao
wameisababishia nchi hiyo madhara na hasara za kiuchumi na kijamii.
Wakati huo huo, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
kupitia msemaji wake, Farhan Haq amezitaka pande zote husika kujizuia
kuchua hatua inayoweza kuvuruga mambo zaidi, na kusisitiza kuwa mgogoro
uliopo unaweza kupatiwa ufumbuzi kwa njia za kisiasa na mazungumzo.
Naye Mkuu wa Umoja wa Afrika, Alpha Conde ambaye pia ni Rais wa
Guinea amesema AU inalaani vikali hatua ya majenerali wa jeshi la
Zimbabwe kutwaa madaraka kwa nguvu na kusisitiza kwamba mfumo wa katiba
unapaswa kuheshimiwa na pande zote.
Huku hayo yakiarifiwa, Morgan Tsvangirai, kinara wa upinzani nchini
Zimbabwe amerejea nchini akitokea Afrika Kusini, kufuatia kile
kinachotajwa kuwa mapinduzi ya kijeshi yasiyo ya umwagikaji wa damu.
Kwa mujibu wa gazeti la NewsDay la Zimbabwe, Tsvangirai ametangaza
kuwa yuko tayari kufanya mazungumzo na Emmerson Mnangagwa, Makamu wa
Rais wa Zimbabwe aliyepigwa kalamu nyekundu na Mugabe hivi karibuni,
kuhusu uundwaji wa serikali ya mpito.
No comments:
Post a Comment