Maandamano ya wananchi ya kupinga serikali
yaliyozusha makabiliano baina yao na polisi jana Jumatatu katika wilaya
za Madjengon na Mabanga katika mji wa Goma mkoani Kivu ya Kaskazini
nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamesababisha vifo vya watu
watano.
Maandamano
hayo ambayo yalijiri jana jioni yaliitishwa na makundi ya wanaharakati
wa kupigania demokrasia na mengineyo kama sehemu ya mgomo mkubwa
unaoshinikiza kuondoka madarakani Rais Joseph Kabila na kudhihirisha
hasira za wananchi kwa kushindwa kuendeshwa uchaguzi wa rais huko Kongo
ili kumchagua rais mpya. Waandamanaji walichoma moto matairi ya gari na
hivyo kusababisha msongamano wa magari katika barabara za mji wa Goma.
Maandamano mengine kama hayo yanatazamiwa kufanywa siku chache zijazo.
Mgogoro wa kisiasa Kongo DR
umesababishwa na hatua ya Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo kukataa
kuachia madaraka baada ya muhula wake kumalizika mwezi Disemba mwaka
jana. Uchaguzi mkuu ulipangwa kufanyika nchini humo kabla ya kumalizika
mwaka huu chini ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya Kinshasa
na mrengo wa upinzani. Hata hivyo imeelezwa kuwa kushindwa kutekelezwa
hatua hiyo si jambo la kushangaza kwa kuzingatia kuwa Tume ya Uchaguzi
ya Kongo mwezi Julai mwaka huu ilitangaza kuwa kuna uwezekano uchaguzi
huo usifanyike mwaka huu kutokana na kuwepo matatizo ya bajeti na
kuendelea machafuko nchini humo.
No comments:
Post a Comment