Rais Uhuru Kenyatta anaongoza kwa asilimia 96
katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa marudio wa urais uliofanyika
Alkhamisi iliyopita nchini Kenya.
Matokeo ya awali ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya
(IEBC) yanaonyesha kuwa Uhuru Kenyatta anaendelea kuongoza kwa kura
zaidi ya milioni 7.
Wagombea wengine wanaomfuata kwa pamoja wamepata chini ya asilimia 5 ya kura zilizohesabiwa kufikia sasa.
Wananchi wa Kenya Alkhamisi walielekea kwenye masanduku ya kupigia
kura katika uchaguzi wa marudio wa urais kufuatia kutenguliwa ule wa
awali uliofanyika Agosti 8 mwaka huu.
Jana Ijumaa, Raila Odinga, kinara wa muungano wa NASA ambao
umebadilishwa jina na sasa litafahamika kama Vuguvugu la Mageuzi NRM
alisema kujitokeza idadi ndogo ya watu katika uchaguzi huo ni ishara
tosha kuwa kulikuwa na uchakachuaji katika uchaguzi wa Agosti 8, huku
akisisitiza kuwa lazima uchaguzi mwingine ufanyike ndani ya siku 90.
Mahakama ya Juu ya Kenya ilitengua matokeo ya uchaguzi huo wa rais
kwa hoja kwamba IEBC ilifanya baadhi ya makosa katika mchakato wa
uchaguzi. Muungano wa upinzani (Nasa) umewahimiza wafuasi wake
kutoshiriki uchaguzi huo baada ya kiongozi wa muungano huo Raila
Odinga kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho.
Katika hatua nyingine, IEBC imetangaza kuakhirisha tena zoezi la
upigaji kura lililotazamiwa hii leo, katika kaunti nne za Kisumu,
Migori, Homa Bay na Siaya, ambazo ni ngome za NASA, ambazo siku ya
Alhamisi wakazi wake hawakupiga kura kwa sababu za kiusalama.
No comments:
Post a Comment